29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

BAKITA YALIA UHABA WA WAKALIMANI

Na HARRIETH MANDARI-

DAR ES SALAAM

WATAALAMU wa lugha ya Kiswahili nchini wameishauri Serikali kuanzisha kozi ya ukalimani katika vyuo vyake ili kuongeza idadi ya wakalimani ambao inadaiwa kuwa ni wachache sana.

Hadi sasa idadi ya wakalimani nchini Tanzania si zaidi ya 20 ambao ni wa kulipwa na wanaotoa huduma katika mikutano mbalimbali ya kimataifa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Seleman Sewangi,  aliliambia MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam kuwa umefika wakati kwa Tanzania kuanzisha kozi hiyo kwa kupata wakalimani wa kutosha wenye uwezo na maarifa katika kukalimani lugha ya Kiswahili kwenda lugha nyingine mbalimbali duniani.

“Hadi hivi sasa Tanzania haina kozi ya ukalimani vyuoni, ni muhimu kuwepo kwa wataalamu wa aina hiyo nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inakua kiuchumi kwa kasi na hivyo kufanya kuongezeka kwa wageni mbalimbali nchini mwetu wakiwemo watalii, wawekezaji na wengine wengi,” alisema Sewangi.

Akaongeza kuwa wapo baadhi ya watu wanaotafsiri lugha ya Kiswahili  wakidhani wanafanya taaluma ya ukalimani jambo ambalo kitaaluma si sahihi na inakuwa vigumu kupata ajira kutokana na kukosa vigezo.

“Kumekuwa na mkanganyiko kuhusu kutafsiri na kukalimani, kutafsiri hata mimi hapa naweza kutafsiri lakini kukalimani ni lazima mtu asomee kozi maalumu ili aweze kutambulika kimataifa,” alisema.

Akaongeza Tanzania kuwe na wakalimani bora na si watafsiri ni lazima wapate mafunzo kwenye vyuo na hivyo kuboresha taaluma hiyo muhimu.

Akichangia kuhusu mchango wa lugha ya Kiswahili katika kuinua sekta ya sanaa nchini, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Geoffrey Mungereza, amesema Kiswahili ni aina ya utamaduni na sanaa ya kujivunia kwa Mtanzania yeyote na umekuza sekta ya sanaa kwa kiasi kikubwa si tu nchini bali hata kimataifa.

“Si tu kwenye sanaa kama muziki lakini hata kwenye filamu nyingi zinatafsiriwa kutoka lugha ya Kiswahili kwenda ya Kiingereza hivyo kufanya hata nchi nyingine kuweza kununua kazi hizo na kufahamu lugha yetu,” alisema Mungereza.

Akatolea mfano wa kipindi cha watoto cha katuni ambacho hurushwa katika  kituo cha televisheni ya Taifa ambapo watoto wanajifunza kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Akawataka vijana kuacha mtizamo wa kuwa kujua Kiingereza ndiyo kuendelela badala yake wajifunze lugha zote muhimu kwa ustawi wao kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles