27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI NAPE HUYO HAPO, WALA HAYUPO MBALI

NILISHAPATA kusema huko nyuma, leo narudia tena; uongozi wa wasanii wetu nchini ni mzuri zaidi kwa sasa pengine kuliko kipindi kingine chochote cha uongozi kwa siku za hivi karibuni.

Kuwapo kwa Waziri Nape Nnauye kwenye wizara inayoshughulikia sanaa (Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) ni sawa na kusema upele umepata mkunaji.

Wasanii nchini mnahitaji nini tena? Tangu mapema Nape ameonyesha nia yake ya dhati ya kuwasaidia wasanii nchini. Tumemshuhudia mara kadhaa kupitia matamshi yake akisema kwamba wasanii wasiwe na wasiwasi kwa sababu yeye (waziri) ni msanii na anapenda kuona mafanikio ya wasanii nchini.

Pengine tungeweza kusema labda waziri alikuwa akizungumza maneno ya kujifagilia tu, lakini sivyo. Anafanya kwa vitendo. Anaishi katika maneno yake.

Kumbukumbu zinaonyesha ni kwa namna gani anapigania haki za wasanii wetu nchini. Hivi karibuni tumemshuhudia akiingia mwenyewe mitaani, maeneo ya Kariakoo na kukamata maharamia wanaodurufu kazi mbalimbali za wasanii wa filamu kinyume cha sheria.

Huyu ndiyo waziri tuliyekuwa tunamtaka. Waziri ambaye anaingia mwenyewe mzigoni kuangalia kuna nini na anatakiwa kufanya nini.

Sanaa iliyokuwa imesahauliwa nchini, sasa tunaona waziri mwenye dhamana akipambana kwa ajili ya haki ya wasanii wake. Wasanii ambao wamekuwa wakilia kila kukicha kuhusu kunyonywa na maharamia wasiojua uchungu wa jasho lao.

Jumatatu ya wiki hii, Waziri Nape ameonekana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwenye mapokezi ya mwigizaji Mike Ezuruonyes ambaye ametua nchini kwa ajili ya kurekodi filamu na wasanii wa Bongo Muvi.

Ni ushirikiano mzuri. Anafanya kazi karibu kabisa na wasanii wenyewe. Mimi namshauri Nape akaze zaidi kwenye eneo la wasanii ambalo lilikuwa limesahaulika.

Lakini hata hivyo asijikite kwenye muziki na filamu pekee. Wizara yake inahusisha utamaduni pia. Viko wapi vikundi vya ngoma? Vipi kuhusu haki na thamani ya waandishi wa miswada ya filamu, vitabu na majarida?

Wale wasanii wa mazingaumbwe na kuruka sarakasi wamepotelea wapi? Nadhani kuna kitu kinatakiwa kufanywa ili kurudisha ari iliyokuwepo awali.

Ni dhamana yako Nape, ambapo pia unapaswa kuwatazama kwa jicho la karibu. Wapo watunzi wa hadithi wazuri sana hapa nchini, lakini kazi zao zinaibwa ovyo na wahuni na kuzidurufu isiyo haki.

Chondechonde mheshimiwa Nape, angaza jicho lako pande zote ili wasanii wote wapate haki zao kupitia wizara yako ambayo kwangu mimi nasema bila shaka kwamba inakutosha!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles