32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MANETO APIGILIA MSUMARI SAKATA LA LEMA

Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

KAULI mbili za majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ambazo zimetolewa kwa nyakati tofauti ndani ya wiki hii, zimeibua mjadala mkubwa ambao sasa umeanza kuhoji weledi na maadili katika vyombo vya kutoa maamuzi, hususani mahakama.

Kauli ya hivi karibuni ambayo ndiyo iliyoibua mjadala huo ni ile iliyotolewa juzi na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Salma Maghimbi wakati akitoa uamuzi wa kutoa haki ya dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Katika maelezo yake, Jaji Maghimbi alisema mahakama ya chini ilishindwa kusimamia mamlaka yake vizuri, hivyo kuingiliwa kabla haijamaliza mwenendo wake.

Jaji Maghimbi ambaye alionya mwenendo huo akisema unanyima watu kupata haki zao, alifafanua kuwa mahakama ikitamka dhamana iko wazi, inatakiwa kukamilisha hilo ikiwa ni pamoja na mshtakiwa kudhaminiwa na kama upande wa pili utakata rufaa kupinga, ufanye hivyo baada ya uamuzi kutolewa.

Kauli hiyo ya Jaji Maghimbi ilitanguliwa na ile iliyotolewa mapema wiki hii na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, Benard Luanda, Jaji Stella Mugasha na Jaji Kipenka Mussa waliohoji kama ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ina wanasheria.

Jopo hilo lilitoa kauli hiyo katika kikao cha kuamua rufani ya Jamhuri dhidi ya Lema juu ya maombi ya dhamana.

Jaji Luanda kwa niaba ya wenzake, alikaririwa akielezea kushangazwa na mbunge huyo kushikiliwa kwa miezi takribani minne bila sababu ya msingi.

 “Tunaomba ofisi ya DPP iwe makini. Mnatuona wanasheria wote hatuna akili. Hivi kweli ofisi ya mwendesha mashtaka haina wanasheria hadi unaitia unajisi taaluma ya sheria?

 “Kazi ya mahakama ni kutatua matatizo na tunataka kuona mtu anatendewa haki kwa misingi ya kisheria,” alisema Jaji Luanda.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kuhusu kauli hizo, Jaji Mstaafu Amir Manento, alisema zinaonyesha kuwapo kwa viashiria vya changamoto ya uzoefu katika mahakama za chini na woga.

Jaji Manento ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), alisema anadhani hayo ndiyo yaliyosababisha mkwamo wa haki ya dhamana kutolewa kwa Lema.

Akifafanua hilo na kile alichokizungumza Jaji Maghimbi, alisema wakati mwingine watu wa mahakama za chini wanakumbana na changamoto za uzoefu na katika mazingira kama hayo ni rahisi kujikuta wakisukumwa na mambo ya kisiasa.

“Kwa sababu yule hakimu kama alivyosema Jaji Maghimbi, ilikuwa akamilishe kwanza kazi ya kwake kwa sababu dhamana alikuwa ameishaikubali na akawa anashughulikia masuala ya kuhakiki wadhamini, sasa ilitakiwa amalize kazi yake wale waombe rufaa dhidi ya uamuzi huo.

“Sasa yule hakimu akaachia katikati kuhakiki wale wadhamini, anaambiwa tayari tumeisha-file notice ya rufaa katika Mahakama Kuu, kawaida angekataa kwa sababu alikuwa ameishamaliza sehemu kubwa ya kuruhusu Lema adhaminiwe, sasa sijui akashtuliwa na kitu gani. Nadhani ni woga fulani ambao hakimu alikuwa nao kwa sababu alikuwa amalize kazi yake yote,” alisema Jaji Manento.

Jaji Manento ambaye amejijengea sifa ya kusimamia kile anachokiamini kuwa ni sahihi katika sheria za nchi, aliongeza kuwa hakimu wa mahakama ya chini alisahau uhuru wake wa kimahakama kwa kudhani atachukuliwa hatua za kisiasa.

“Hakimu angemaliza kazi yake yote ya kuhakiki wadhamini wakasaini bondi kimahakama… yaani huko nje polisi wangemkamata angekuwa nje ya dhamana, lakini hakimu aliogopa kutekeleza wajibu wake, hilo siwezi kujibu… kumekuja mambo ya kisiasa mno, nadhani yule hakimu akasahau ule uhuru wake wa kimahakama kuwa hata akitoa dhamana hataweza kuchukuliwa hatua za kisiasa,” alisema Jaji Manento.

Kutokana na kauli za wataalamu hao wa sheria kuelekeza lawama Ofisi ya DPP, MTANZANIA Jumapili lilimtafuta kwa simu Mkurugenzi wake, Biswalo Mganga, ambaye hata hivyo alikataa kuzungumza lolote, zaidi akimtaka mwandishi ampelekee nakala ya uamuzi wa majaji hao kwa lengo la kuisoma ili atoe majibu.

“Kitu cha kwanza simjui ninayeongea naye na yuko mbele yangu simjui anafanya nini. Kama unao uamuzi huo niletee ofisini kwangu ili nisome kama hayo uliyouliza yamo, kisha nitatoa maoni yangu kwa sababu taratibu zipo wazi,” alisema Mganga.

Awali gazeti hili lilimtafuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, lakini  hakupatikana kutokana na simu yake kuita muda wote kila ilipopigwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu. Gazeti hili linaendelea kumtafuta.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amos Mpanju, alipotakiwa kuzungumzia mkanganyiko huo wa dhamana ya Lema, alisema mahakama ni mhimili unaojitegemea, hivyo kutaka mambo hayo yaliyoibuliwa yazungumzwe katika ngazi hiyo.

“Moja siwezi kuliongelea kwa sababu nyingi tu, la kwanza liko wazi kwamba mahakama ni mhimili unaojitegemea na hayo mamlaka imepewa kwa mujibu wa Katiba, kama unataka kusoma angalia ibara ya nne, pia  angalia ibara ya 107,” alisema.

Alisisitiza kuwa wenye uwezo wa kuliongelea jambo hilo ni mahakama, lakini kwa upande wa wizara haina mamlaka ya kuliongelea hilo.

“Mahakama wao ndio wanaweza wakakwambia maamuzi yao au taratibu zao, sisi watu wa wizara hatuwezi kuliongelea hilo, si mimi, si waziri kwa sababu sisi kuja kuliongelea kwa sababu ya kisera kutoa ufafanuzi, lazima maelezo ya kitaalamu yatoke kule endapo kimsingi jambo hili litatuhitaji sisi,” alisema Mpanju.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles