32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

FANYA MICHONGO YOTE, LAKINI SIYO MADUDE

Na JOSEPH SHALUWA

MFALME wa Pop duniani, hayati Michael Jackson ‘MJ’ alifariki dunia Juni 25, 2009. Ndoto zake zote zilizimikia hapo.

Chanzo cha kifo chake kinaelezwa ni kuugua, pamoja na maradhi mengine MJ alikuwa akikabiliwa na msongo wa mawazo na matatizo ya kisaikolojia yaliyopelekea kupatwa pia tatizo la akili.

Lakini nyuma ya pazia inadaiwa kuwa, MJ alifariki baada ya kuzidisha kipimo cha dawa za kulevya wakati akiwa katika hali ya ugonjwa huku akitumia dawa maalum za kutuliza maumivu makali.

Maelezo ya daktari wake binafsi, Dk. Conrad Murray yanafafanua kuwa MJ alikuwa katika hali ya kukosa usingizi, iliyosababishwa na madawa makali ya kuzuia maumivu makali aliyokuwa akiyapata siku 60 za mwisho wa uhai wake.

Hata hivyo, maelezo mengine ya Dk. Murray yanaeleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni sababu nyingine iliyochangia kifo cha staa huyo mwenye rekodi ya ajabu kwenye muziki wa Pop duniani.

Tuachane na Michael Jackson. Hapa nchini wapo mastaa kadhaa ambao maisha yao yameharibika kabisa mara baada ya kutopea kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Wapo wengine waliodaiwa kufariki kutokana na kuathirika vibaya na dawa hizo. Kila mtu anasema lake, lakini ukweli ni kwamba dawa za kulevya ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Kuna waliokuwa wanamuziki wakali kabisa, wenye sauti tamu lakini mara walipogusa tu dawa za kulevya vipaji vyao vikaporomoka na ukawa mwisho wao. Wengine leo hii wanajaribu kuibuka tena. Rehema Chalamika ‘Ray C’ anaweza kuwa mfano mzuri.

Kama mfano huo hautoshi, yupo Chid Benz. Yule mwenye sauti tamu, nzito, inayosisimua. Leo yuko wapi? Naye anadaiwa tatizo ni madude.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitaja orodha ya watu wanaotuhumiwa kwa matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya. Walitajwa wengi wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara na wasanii.

Kati ya wasanii waliotajwa ni pamoja na staa wa kunogesha video za wasanii, Agnes Gerald ‘Masogange’, mwigizaji Wema Sepetu, Mbongo Fleva Rashid Makwilo ‘Chid Benz’, Khaleed Mohamed ‘T.I.D’ na wengine.

Mashauri ya baadhi ya watuhumiwa hao yanaendelea mahakamani. Lakini nataka kuzungumza kidogo na jamii ya wasanii wa Bongo kuhusiana na matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya.  

Ipo mifano mingi inayoonyesha madhara ya moja kwa moja ya kutumia au kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

 

UTUMIAJI

Athari za dawa za kulevya zipo wazi kabisa, hakuna aliyeingia kwenye utumiaji akapata matokeo chanya. Ni kujidanganya kwamba eti kwa kutumia mihadarati utapata stimu zaidi za kufanya vizuri kwenye sanaa.

Zaidi waliotumia tunawaona sasa hivi wakiwa kwenye mateso makubwa. Wamepoteza uwezo wao kisanii, wamekuwa wagomvi, wengine wamepoteza haiba zao na wamedhoofu kabisa miili yao.

Kwa sasa wamekuwa tegemezi na zaidi wanatafuta tiba za kukabiliana na kuacha matumizi ya madawa hayo. Kumbuka kuingia ni rahisi sana, lakini kuacha ni mzigo mzito.

Ni afadhali ambaye hajawahi kutumia, akaachana kabisa na wazo hilo. Hakuna cha maana atakachopata zaidi na majuto. Kama hujawahi, kaa mbali – usithubutu kabisa.

 

USAMBAZAJI

Kila mmoja anaelewa kinachompata mtu anayekutwa na hatia ya kusambaza dawa za kulevya. Ni kifungo jela. Maana yake ndoto zako zote zinazimika mara moja.

Wapo Watanzania kadhaa ambao wamekamatwa nje ya nchi na wanatumikia vifungo vyao hukohuko kutokana na kukutwa na dawa za kulevya.

Kimsingi athari ni kubwa, maana ukiachana na hiyo, wale wanaotumiwa kama punda kwa kumezeshwa dawa hizo na kusafiri nayo, kuna matatizo makubwa kiafya yanayoweza kumkuta mhusika ikiwemo kifo.

 

UJANJA NI NINI?

Vijana wa sasa wanaamini ujanja ni pesa. Yaani mtu akishakuwa na fedha za kutosha, basi kunakuwa hakuna mjanja kama yeye. Ni kweli. Fedha ni kila kitu, lakini si kila njia ya kupata fedha ni salama.

Achana na shotikati. Ujanja ni ubunifu. Lazima kijana uwe mbunifu, ufikirie nini ufanye ili uweze kufanikiwa kifedha. Kama ni mwanamuziki imba zaidi. Toa tungo kali, utatoboa.

Kama ni msanii tafuta watu wenye mawazo mazuri ya hadithi, chagua wasanii wenye vipaji, wekeni kambi. Mkitoka mtakuwa na sinema nzuri ya kusisimua ambayo inaweza kubadili maisha yako. Siyo kuhangaika na madude!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles