25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TARATIBU TUTAZOEA MFUMO WA KUNUNUA BURUDANI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

TUMEENDELEA kushuhudia muziki wa Bongo Fleva ukipata masoko mapya ya bidhaa zake. Hivi sasa ni rahisi msanii anapotoa wimbo hasa audio kuipeleka kwenye maduka ya kimtandao ili mashabiki waupakue kwa kuchangia fedha kidogo.

Jumatano wiki hii Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel, alifanya uzinduzi wa tovuti mpya ya Afro Premiere inayojihusisha na biashara ya kuuza video za wasanii wa muziki mtandaoni.

Huu ni mwendelezo wa mapinduzi ya biashara kwenye muziki wa Bongo Fleva, ambapo hapo awali wasanii waliuza audio pekee na kuacha fedha nyingi zikipotea katika upande wa video.

Inafahamika kabla ya kuanza kutumia masoko kama haya ya kimtandao, wasanii walitegemea zaidi maonyesho licha ya muziki kutoa burudani kwa mashabiki eneo lolote walilopo ukiacha kwenye hayo matamasha.

Sehemu kubwa ya maisha yetu inatawaliwa na muziki, ambao umekuwa ukitoa msaada kwa watu wenye msongo wa mawazo pale wanapohitaji kuliwazwa hata kwenye matumizi mengine muziki umeendelea kuwafariji watu.

Sasa kama muziki ni huduma kwanini usilipie mfano wa zile huduma nyingine muhimu? Ni jambo geni kwetu ndiyo maana hata mfumo huu mpya wa kulipa shilingi 300 ili utazame video ya msanii umepokelewa kwa mitazamo tofauti.

Hivi ni nani ambaye hajui wasanii wanawekeza muda na fedha nyingi katika uandaaji wa video? Tumekuwa tukishuhudia jinsi wana Bongo Fleva wakisafiri kutoka hapa nchini kwenda Afrika Kusini kufanya video kwa bei ya juu.

Uandaaji wa video nzuri umekuwa ghali kuliko audio ndiyo maana mfumo huu ulipotambulishwa kwa mara ya kwanza nilijikuta mwenye furaha sababu nafahamu matatizo wanayoyapata.

Nilichokipenda zaidi kwenye mfumo wa Afro Premiere ni kwamba, umeweka uwiano sawa wa mapato kati ya msanii, prodyuza na Serikali.

Hapo unaweza kuona namna waandaaji wa muziki walivyokumbukwa kwenye mfumo huu maana kumekuwa na vilio vingi kutoka kwa watayarishaji wa muziki kutupwa na wasanii wao pale wanapomaliza kazi yao.

Na jambo jema ni kwamba, upo wazi na mamlaka ya mapato itakuwa inachukua kodi yake bila kificho na hapo sasa muziki wetu utapanda thamani na kila anayehusika na muziki atanufaika. Hongera G Nako, Jux, Roma, Baghdad kwa kuanza kutumia fursa hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles