28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA AGOMA KUJIBU TUHUMA ZA MITANDAONI

Na AGATHA CHARLES, DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema majibu ya tuhuma anazotuhumiwa katika mitandao ya kijamii yanapatikana huko huko mitandaoni.

Kauli hiyo aliitoa ofisini kwake, Dar es Salaam jana, wakati wa kupokea ripoti ya utendaji kazi ya kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi iliyotolewa na wanasheria wa kujitolea waliofanya kazi katika wilaya tofauti jijini Dar es Salaam.

Majibu hayo ya Makonda yalitokana na swali la mmoja wa waandishi wa habari aliyemtaka azungumzie tuhuma zinazomhusu, ikiwamo kughushi cheti cha elimu yake ya sekondari inayoendelea katika mitandao ya kijamii.

“Hayo ya mitandao ya kijamii yanajibiwa kimitandao ya kijamii, ukienda huko utapata majibu, siko hapa kupoteza focus (mwelekeo). Ukiona maneno yanakuwa mengi kuhusu dawa za kulevya ujue vita ni kubwa, imefika penyewe,” alisema.

Tangu Makonda alipojikita kushughulikia wanaodaiwa kuuza, kusambaza na kutumia dawa za kulevya kwa kuwataja hadharani, wakiwamo wasanii, wanasiasa na wafanyabiashara na kuwataka kujisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, amekuwa akituhumiwa kwa mambo kadha wa kadha.

Moja ya tuhuma zilizoibuka hivi karibuni katika mitandao ya kijamii ni kuhusu kile kinachodaiwa kuwa utata wa majina yake anayoyatumia na hivyo kudaiwa kughushi vyeti vyake.

 

Kabla ya tuhuma hizo, pia Makonda alidaiwa kumiliki mali, ikiwamo jengo la ghorofa na gari la kifahari zilizotolewa bungeni na Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la Msukuma.

 

 

Awali, katika mkutano huo, Makonda alisema wanasheria 35 ndio walihusika katika kutoa msaada wa kisheria bure katika wilaya za Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo na Kigamboni kwa kipindi cha kuanzia Desemba 16, mwaka jana hadi Februari 24, mwaka huu.

Kiongozi wa wanasheria hao, Georgia Kamina, alisema walifanikiwa kuwahudumia wananchi 10,217 na kutoa msaada katika kesi 701, zikiwamo zilizohusisha mirathi, ndoa, ajira na migogoro ya ardhi.

Alisema Ilala ilipatiwa msaada wa kisheria katika kesi 266, Temeke 200, Kinondoni 180, huku changamoto ikiwa ni uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kisheria.

“Moja ya kesi tulizokutana nazo ni iliyokuwa ya mirathi ambayo mhusika alizungushwa kwa miaka 10 bila kutolewa uamuzi kutokana na faili lake kupotea, lakini baada ya kufuatilia kwa kina faili lilionekana na mama huyo alipatiwa mali zake. Wengine waliopatiwa msaada ni vibarua zaidi ya 200,” alisema Kamina.

Akizungumzia hilo, Makonda aliwapongeza na kutoa wito kwa wanasheria wengine kuwa na moyo wa kusaidia wanyonge na si wahalifu.

“Wanasheria wafanye kazi kusaidia wanyonge, nitajisikia vibaya mwanasheria akimsaidia mhalifu badala ya mnyonge. Kama muda kidogo tu watu wote hao wamehudumiwa, tuendelee kujenga baada ya mwaka tutaona mafanikio makubwa,” alisema Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles