26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Manji ampandisha kizimbani kigogo Simba

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

UPINZANI wa watani wa jadi, Simba na Yanga umehamia mahakamani baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, kumpandisha kizimbani Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Musleh Al Rawah, akidaiwa kumpiga mwanaye.

Mjumbe huyo wa Simba alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, alisomewa shtaka la kumjeruhi mtoto wa Manji, Mehboob Manji.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Genis Tesha, alidai kuwa Al Rawah alifanya kosa hilo, Machi 8, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa uliopo Chang’ombe, baada ya kumalizika mchezo wa watani wa jadi ulioisha kwa Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya Yanga.

Tesha alidai kuwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa Al Rawah alimpiga teke Mehboob katika sehemu mbalimbali za mwili ukiwamo uso na kumsababishia majeraha mazito.

Al Rawah ambaye ni mfanyabiashara na raia wa hapa nchini anayetetewa na Wakili Dk. Damas Ndumbaro, alikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ukadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hawapingi dhamana kwa mshtakiwa.

Kwa upande wa Wakili Ndumbaro, naye aliomba mteja wake apewe dhamana.

Hakimu Moshi akitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo, alimtaka awe na mdhamini mmoja ambaye anatoka katika taasisi inayotambulika ama serikalini.

Baada ya mdhamini kujitokeza, upande wa mashtaka ulifanyia uhakiki barua yake ndani ya saa moja kama ilivyoelekezwa na mahakama na mshtakiwa akaachiwa huru.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 20, mwaka huu kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika ama la.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles