25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

OSTAZI JUMA NA MUSOMA ANAJIFUNZA NINI KWA FELLA, TALE NA SALLAM SK?

KUNA watu wamepata umaarufu katika namna ya kuchekesha kidogo. Unamkumbuka yule aliyejiita Mganga wa Diamond? Katika namna isiyotarajiwa, eti ghafla na yeye akawa maarufu tena maarufu sana. Kila eneo akasifika. Kuanzia kwenye blog, magazeti hata katika baadhi ya vipindi vya televisheni akawa anatajwa kila wakati. Ila sasa yuko wapi? Yale maneno na ahadi alizotoa juu ya Diamond ziko wapi? Diamond bado anashikilia usukani wa Bongo Fleva huku yeye akiwa taabani.

     Kama wengine na yeye pia alikuwa katika mbio za kusaka umaarufu na jina bila kutoa jasho. Nahisi alifanikiwa.

   Siyo huko tu. Hayo yapo katika siasa, muziki hata filamu. Si yupo yule mwanasiasa aliyesema kama akichaguliwa bangi na mirungi itaruhusiwa? Na yupo yule mwingine badala ya kuuza sera zake, akaanza kujitapa kuwa anakaa Masaki na yeye ni mmoja kati ya watu matajiri Tanzania. Wa aina hiyo wapo.

 

  Kila eneo wapo. Wengine baada ya kuona kila eneo limejaa wamejipachika umeneja na uongozi maeneo fulani. Si unamjua Ostaz Juma na Musoma.

     Leo nimemkumbuka sana. Si unakumbuka kama alikuwa ni bosi fulani, pedeshee fulani na pia akajifanya mwanamuziki fulani?

   Sitaki kuzungumzia alichowahi kukifanya kwa PNC. Ila angalia utendaji wake wa kazi kama meneja wa wasanii. Tangu alipowahi kuwachukua wakina Dogo Janja, Suma Mnazaleti, Amazoni na wengineo, kipi kikubwa alikifanya katika kuendeleza uwezo na vipaji vya wasanii hao?

   Hata kwa jicho la kinyonga, unaweza kumfananisha Ostazi Juma na Musoma na Said Fella? Muangalie Aslay. Hukumu kipaji chake, kisha muangalie Dogo Janja wa kipindi cha Ostaz Juma pia hukumu kipaji chake. Wote hawa wawili wana vipaji vikubwa sana. Ila mmoja alikuwa kwa mtu makini na mwingine alikuwa na mtu mzushi ndiyo maana maendeleo yake kimuziki yalidumaa mpaka aliporudi tena kwa wanaojua kazi zao.

   Kumiliki visenti kadhaa siyo tiketi ya kuwa meneja wa watu. Wenye uwezo na kazi hiyo wapo. Wakina Babu Tale wapo, wakina Alex Msama wapo. Hizi sifa na kutaka kuonekana fulani ana pesa zisishabikiwe sana hata kufanya vijana wenye vipaji ambavyo kimsingi ndiyo mkombozi wa maisha yao viishie kupotea.

   PNC sio msanii mdogo. Tangu kitambo anafanya vizuri na ana ‘fan base’ kubwa tu. Ila kuna tatizo katika ukuaji wake wa muziki. Mbali na yeye mwenyewe kukosea katika mambo fulani, ila pia hata uongozi wake chini ya Ostazi Juma na Musoma ulimpotezea kabisa dira.

      Zaidi ya kumsaidia hela mbuzi, Ostazi Juma kamsaidia kipi cha maana PNC? Au kumdhalilisha baada ya PNC kuhitaji msaada na kuweka hadharani ile video na jamii yote ijue ana matatizo, ndiyo msaada kwa anavyoamini?

   Wakina Chief Kiumbe wana hela. Ila hata siku moja hatujawahi kuwasikia wakiwadhalilisha wakina Matonya au Tunda. Tofauti ipo. Kati ya uongozi bora na uongozi magumashi, tofauti ipo.

    Dhima halisi ya meneja ni kumfanya muhusika akue kisanaa na sanaa iweze kumletea mafanikio halisi. Sio kumpa pesa mbuzi kisha kumdhalilisha.

   Kwa watu aina ya Ostazi Juma, hata wangekuwa na wasanii aina ya Diamond, Barnaba na Ali Kiba, bado wasanii hao wasingeweza kufanya vizuri. Kwani tatizo haliko kwa wahusika wenyewe bali tatizo liko kwao kama mameneja.

   Jaribu kumtafakari Dogo Janja wa Tip Top, kisha mtafakari alipokuwa Mtanashati. Wanafanana? Labda wa Tip Top hakuwa amewahi kwenda Afrika Kusini wala kutoka Arusha kwa ndege ila wa Mtanashati alienda. Ila ni nani alikuwa akitambulika zaidi kimuziki? Ni nani alikuwa akionekana kuwa ni nyota hatari ya baadaye? Kati ya Babu Tale na Ostazi Juma, tofauti ipo.

   Suala sio fedha, ila ni namna gani unatumia vizuri fedha na akili yako kumfanya fulani aweze kufikia malengo yake. Katika hili Ostazi Juma alishindwa vibaya sana. ni kheri alivyowaachia wakina Fella wafanye kazi yao.

   Eti katika hali kabisa ya ubinadamu na kujali, unaweza vipi kumdhalilisha mtu kama alivyomfanyia PNC kisha kusema kuwa wanastahili kufanyiwa hivyo? Hawa watu ni virusi katika sanaa yetu.

   Hivi kama angekuwa anawaazima wasanii magari na kuwapangishia majumba kama anavyofanya Chief Kiumbe, ingekuwaje? Nina hofu siku moja angemtoa nje mtu usiku.

   Haikuwa ujanja alichofanya Ostaz Juma kwa PNC. Kwa watoto wa mjini, waliokulia mitaa fulani ya mjini na kucheza hapa hapa town, kwao kitendo kile wanakiita cha kishamba huku waerevu wanakisema kuwa ni cha kilimbukeni. Leo nilimkumbuka sana huyu Meneja Magumashi

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles