Na Muhammed Khamis (UoI)
MKUTANO wa tisa kikao cha tano cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), unatarajiwa kuvuta hisia kali kwa wananchi na viongozi wa Serikali kutokana na kuwasilishwa kwa hoja binafsi ya dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa Baraza hilo, Raya Issa Mselem alisema kikao hicho kinatarajiwa kuanza kesho.
Alisema kila mmoja, sasa ni shahidi juu ya jitihada zinazofanyika Tanzania Bara za kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kuathiri kwa kiasi kikubwa makundi ya vijana.
‘’Kutokana na hali hii, huwenda wajumbe wa baraza hili kupitia Mohamed Said Mohamed wameiona ipo haja ya kuwasilishwa hoja ili kuwekwa sheria kali zitakazozuia matumizi ya dawa hapa Zanzibar,’’alisema Raya.
Alisema miswada mingine itakayowasilishwa ni pamoja na muswada wa kufuta sheria ya nembo namba 1 ya mwaka 1985 na sheria ya Zanzibar nembo ya Serikali na wimbo wa Taifa wa Zanzibar.