27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MNAOSHANGAA DIAMOND KUPEWA BENDERA YA TAIFA VEEPE?

DIAMOND BENDERA

Na MARKUS MPANGALA

NILIPOONA tangazo la waandaji wa michuano ya soka barani Afrika CAF, kuhusu mwanamuziki Nasib Abdul maarufu kama Diamond kutumbuiza kwenye mashindano hayo, upesi nilijikuta natabasamu.

Ndiyo, nilikuwa na furaha kwakuwa niliona imekuwa fursa ya kipekee mno kwa mwanamuziki wa Bongo Fleva.

Kutokana na hatua hiyo ndipo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimkabidhi Bendera ya Taifa mwanamuziki huyo wakati akimuaga kabla ya kuelekea kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON.

Mashindano hayo yanafanyika nchini Gabon na yatazinduliwa leo Jumamosi na kuzikutanisha nchi mbalimbali pamoja na mastaa wanaocheza soka huko barani Ulaya.

Wapo badhi ya Watanzania wenzetu wamehoji ni kwanini Waziri amemkabidhi bendera mwanamuziki huyo?

Wanasema kwanini amkabidhi mtu ambaye anakwenda kuburudisha tu kwenye mashindano ya AFCON? Na zaidi wanasema haikuwa jambo sawa kumkabidhi bendera hiyo.

Binafsi ninaamini wanaoshangazwa au kuhoji wamekosa kuelewa mambo madogo tu. Tunafahamu kuwa muziki wa Bongo Fleva umepiga hatua kubwa sana barani Afrika na anga za kimataifa.

Tunafahamu miongoni mwa mabalozi wazuri wa muziki huu ni AY, Diamond, Ali Kiba, Lady Jaydee, Mwanafalsafa na wengineo wengi na wasijali hata kama sijawataja.

Baadhi ya Watanzania wanaohiji hilo ninapenda kuwaeleza mambo muhimu ambayo tunatakiwa kuyajua na kutilia mkazo juu ya shavu alilokula Diamond.

Mosi, katika hali ya kawaida utagundua kuwa suala la Diamond kutumbuiza kwenye mashindano ya AFCON ni moja ya fursa muhimu mno katika anga za michezo na burudani, pamoja na shughuli zake binafsi kama mwanamuziki na wanamuziki wa Bongo Fleva kwa ujumla wake.

Kwamba mwanamuziki huyo ameshiriki tuzo mbalimbali barani Afrika na huko Ughaibuni. Diamond ametumbuiza kwenye majukwaa makubwa ya kimataifa akishirikiana na wanamuziki wakubwa pia kama Davido.

Pili, Diamond amefanikiwa kujenga ushindani mkali wa kimuziki na baadhi ya mastaa wa Nigeria, nchi ambayo imekuwa na ujivuni mkubwa kwenye muziki.

Lakini sasa mwanamuziki wa Kitanzania amekabidhiwa fursa ya kutamba jukwaani, kunogesha nyimbo zake na kuwaburudisha wanamuziki, wageni waalikwa, wanasoka na maofisa mbalimbali.

Tatu, tenda aliyopata Diamond kutumbuiza kwenye mashindano ya AFCON anawakilisha utaifa wa Tanzania na anastahili kupeperusha bendera hiyo.

Ikumbukwe juhudi zake binafsi na sapoti ya mashabiki hapa nchini imemfikisha katika ngazi za juu.

Yeye kama raia wa Tanzania anastahili kuliwakilisha vema Taifa. Wakati fulani Diamond aliwahi kutania alipoandika mtandaoni kuwa: ‘Hata ukipata mpenzi ambaye ni raia wa nje, unatakiwa kuiwakilisha vema nchi yako,’ ilikuwa kauli ya utani lakini ndiyo msingi wa hoja pia.

Nne, hakuna mwanamuziki wa Tanzania aliyepata kutumbuiza kwenye Mashindano ya AFCON, kupewa fursa hiyo ni jambo la kujivunia kama Diamond mwanamuziki binafsi na kama nchi pia.

Ni suala la mkakati wa sifa ya nchi ndiyo maana waziri aliwajibika kumkabidhi bendera hiyo. Tofauti yetu ni kuvielewa vitu vya kujivunia ndani ya taifa ndiyo maana wengine wanadhani bendera hukabidhiwa kwa watu wanaokwenda kushindana kama soka, kikapu, netboli, ngumi na kadhalika.

Tano, kuaminika katika ubora kunambeba Diamond. Huwezi kupewa tenda ya kutumbuiza mashindano makubwa ikiwa huaminiki kiuwezo, nidhamu na mengine muhimu yanayokupa sifa.

Sita, suala la uchumi linaingia pia kwani Diamond amepewa kazi ambayo itakuwa ikiweka alama ya kuutangaza muziki wa Bongo Fleva.

Malipo anayopata yanamgusa moja kwa moja kuanzia house girl, saluni, waosha magari, vyombo vya habari na waandishi na Watanzania kwa ujumla.

Saba, mwisho niwakumbushe wasanii Jennifer Lopez (Marekani) alitumbuiza kwenye Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil. Shakira alitumbuiza mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na 2014 kule Brazil.

Tunaweza kusema Colombia na Marekani zimeshiriki Kombe la Dunia, lakini hatuwezi kukwepa ukweli kuwa wasanii hao wamefika hapo kwa staili hii ya Diamond ya kuwakilisha nchi zao licha ya muziki wao kukonga nyoyo za washabiki.

Changamoto inabakia kwa wanamuziki wengine wa Bongo Fleva, wanajifunza nini kwa Diamond? TFF inajifunza nini kwa Diamond? Hayo ni maoni yangu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles