27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MKEMIA MKUU AFICHUA SIRI VIFO VYA SUMU, ULEVI

sampuli

Na AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM 

IDADI ya watu wanaohusishwa kufariki dunia kwa sumu imeongezeka katika kipindi cha mwaka 2015/2016 na kufikia 80 ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) baada ya kupokea sampuli kutoka katika vyombo vilivyoruhusiwa kisheria ikiwamo Jeshi la Polisi na hospitali, idadi ya waliohusishwa kufariki dunia kwa sumu mwaka 2014/2015 ni 76 na mwaka 2013/2014 ni 69.

Kwa takwimu hizo, idadi ya watu waliohusishwa kufariki dunia kwa sumu katika kipindi cha miaka mitatu iliyoishia Juni, mwaka jana imefikia 225.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili ofisini kwake Dar es Salaam juzi, Mkemia  Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, alisema ofisi yake kupitia Kitengo cha Kuratibu Matukio ya Sumu (NPCC) imepokea majalada 436 yenye sampuli 1,237 katika kipindi cha miaka mitatu.

“Majalada yaliyopokelewa yaliyohusishwa na sumu kwa mwaka 2013/2014 yapo 69, mwaka 2014/2015 yalikuwa 76 wakati mwaka 2015/2016 tumepokea majalada 80,” alisema.

Manyele alisema hadi sasa majalada 346 ambayo ni sawa na asilimia 80 yameshafanyiwa uchunguzi wakati asilimia 20 ya majalada yanaendelea kuchunguzwa.

Alisema kati ya majalada 436 yaliyopokewa ofisini kwake, yanayohusu madhara ya sumu kwa kutumia sampuli mbalimbali yalikuwa ni asilimia 48 wakati yaliyohusu vifo vya binadamu yalikuwa ni asilimia 52.

“Sampuli zinazotumika ni viungo vya binadamu, unaweza ukakuta jalada moja linafanyiwa uchunguzi kwa kutumia zaidi ya sampuli moja hadi mbili, unaweza ukaamua kuchukua mfano ini na figo kwa mtu mmoja,” alisema.

Manyele alisema kati ya majalada hayo  yaliyofanyiwa uchunguzi, yapo yenye sampuli zilizohusisha vifo vya binadamu vilivyotokana na sumu mbalimbali  ikiwamo pombe na mimea.

Alisema katika majalada hayo, sampuli 100 zilibainika kuwa na sumu. Kwa mwaka 2013/2014 zilikuwa 30, mwaka 2014/2015 zilikuwa 33 na mwaka 2015/2016 zilikuwa 37.

“Sumu zilizobainika katika sampuli hizo ni pamoja na viuatilifu, ikiwamo dawa za kuulia wadudu wanaopatikana katika mahindi na nafaka nyinginezo zilizodhuru kwa asilimia 58.

“Kati ya sampuli 58 zilizotokana na viuatilifu hivyo, kwa mwaka 2013/2014 zilikuwa 21, mwaka 2014/2015 zilibainika sampuli 16 wakati sampuli 21 zilipatikana kwa mwaka 2015/16,” alisema.

Mbali na hilo, alisema katika kipindi hicho sampuli 12 zilibainika katika pombe. Mwaka 2013/2014 zilikuwa tano, mwaka 2014/2015 zilipatikana tatu na mwaka 2105/2016 nne.

Pia alisema sampuli zilizopatikana na alkaloids (kemikali inayopatikana katika mimea, inayotengenezwa viwandani na dawa za kienyeji) zilikuwa 42.

“Mwaka 2013/2014 sampuli zilizobainika kuwa na alkaloids zilikuwa 10 na mwaka 2014/2015 zilikuwa 15 wakati mwaka 2015/2016 zilikuwa 17,” alisema.

Alisema sumu nyingine zilizopatikana katika sampuli hizo zilikuwa jumla 20. Kwa mwaka 2013/2014 zilikuwa saba, mwaka 2014/2015 tisa na mwaka 2015/2016 nne.

Aliongeza kwa kusema kuwa ongezeko la watu kula vyakula vinavyohusishwa na sumu linatokana na shughuli za kijamii kama kilimo na viwanda ambazo zinafanywa na binadamu kila siku.

“Wananchi wanapaswa wafahamu ofisi ina kituo cha kudhibiti sumu, sumu hizi zinatokana na shughuli zetu za kila siku kama kilimo na viwanda, hivyo watu wanapaswa kujua jinsi ya kujikinga na kudhibiti.

“Sisi kama ofisi hatua ya kwanza tunahakikisha tunazuia kemikali hatari kuingia nchini na hata kama zinahitajika kwa matumizi, tunatafuta mbadala wake,” alisema.

Manyele alisema asilimia kubwa ya watu waliobainika kula sumu pindi wanapofanyiwa uchunguzi wanakutwa ni kutokana na kasoro mbalimbali katika ulaji na kuchanganya dawa za kutibu magonjwa ya binadamu na pombe.

“Unaweza ukakuta mtu amekufa, lakini pembeni kuna chupa ya pombe, ukimfuatilia unaambiwa alikuwa mgonjwa, hapo ni wazi unaona kuwa kifo chake kimetokana na kuchanganya dawa na pombe,” alisema.

Manyele alisema zipo kesi zinazohusisha ulaji wa vyakula bila mpangilio, huku kundi jingine likishindwa kuwahi kujipa huduma ya kwanza baada ya kunywa vitu vyenye madhara yanayofanana na sumu kama mafuta ya taa.

“Tumeanzisha utaratibu wa kuhakikisha kitengo hiki cha sumu kinawasaidia wananchi, kwa sasa tumeweka utaratibu wa wananchi kupiga namba za simu na kueleza shida zao.

“Mfano watu wanaokunywa vitu vyenye sumu kama mafuta ya taa, dawa za kuua wadudu na nyinginezo, wote tunawapa maelekezo jinsi ya kufanya ili wasipate madhara,” alisema.

Pia alisema ofisi hiyo inashirikiana na hospitali mbalimbali ili kusaidia kupata taarifa kwa haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles