Na Amina Omari-Handeni
JAMII ya wafugaji wa Kata ya Kwamagome wilayani Handeni, wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro wa ardhi wa uuzaji wa eneo la malisho la zaidi ya ekari 100.
Eneo hilo hapo awali lilitengwa maalumu kwa ajili ya malisho ya mifugo pamoja na njia ya maji na uongozi wa Serikali ya kata kuamua kuliuza kwa wakulima.
Wakizungumza na MTANZANIA jana wafugaji hao walisema kuuzwa kwa eneo hilo kumesababisha kuwepo kwa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mmoja wa wafugaji hao, Philipo Lutipo, alisema eneo la malisho limeuzwa na sasa hakuna maeneo ya malisho ya mifugo yetu bali eneo lote limegeuzwa na kuwa mashamba.
“Tunaomba Serikali itusaidie kupata haki yetu ya ardhi kwani uongozi wa wilaya uliweka utaratibu mzuri wa maeneo ya wakulima na wafugaji, lakini viongozi wa Serikali ya kata wameyauza kinyemela,” alisema Lutipo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, alisema tayari ameunda kikosi kazi cha kushughulika na kero za uuzaji kiholela wa ardhi.
“Suala la Kwamagome lipo kinadharia mezani kwangu, tayari nimeunda kikosi kazi ambacho kifanya utafiti ili kuweza kubaini viongozi waliohusika na kuwachukulia hatua za kinidhamu,” alisema DC huyo.