30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

GREEN MAMBA: NYOKA MMBEA ANAYEPENDA KUSIKILIZA MAONGEZI YA BINADAMU

Mmoja wa watalii akijaribu kumshika nyoka kutoka kwa Mhifadhi, Nesto Hassan wa Kaole.
Mmoja wa watalii akijaribu kumshika nyoka kutoka kwa Mhifadhi, Nesto Hassan wa Kaole.

Na Esther Mbussi-Dar es Salaam

INAFAHAMIKA kuwa nyoka ni mnyama hatari anyeogopwa na wengi hasa wanawake.

Nyoka anaogopwa kwa kuwa wengi wanaamini ana sumu kali inayoweza kuua tena kwa muda mfupi baada ya kukudhuru.

Wako nyoka wa aina nyingi, wengine wana sumu kali na wengine hawana kabisa, pia wana tabia tofauti kulingana na jamii (specie) yake.

Katika Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani Kijiji cha Kaole, Kilomita sita kutoka Barabara kuu ya Bagamoyo, iko hifadhi ya nyoka inayoitwa Kaole Snake Park and Leisure.

Ndani ya hifadhi hiyo inayomilikiwa na Mtanzania, kuna nyoka wa kila aina, ndege kama kanga, bata bukini, bundi, vinyonga, kenge, kobe na viumbe hai vingine.

Kwa kuwa hifadhi hiyo ni mpya kwani imefunguliwa Novemba mwaka huu, wageni wanaotembelea bado si wengi.

Kivutio kikubwa katika hifadhi hii ni nyoka ambao wametengwa kila mmoja katika banda lake ambapo kila mmoja ana tabia yake akiwamo nyoka mbea.

Mhifadhi katika hifadhi hiyo, Nesto Hassan anasema katika hifadhi hiyo kuna nyoka wa kila aina akiwamo mkubwa kabisa anayeweza kula mbwa au binadamu.

Anasema baadhi ya nyoka kama ‘ruvous’ hana sumu na ndiye anayetumika na waganga wa kienyeji na wanaofanya mazingaombwe.

“Nyoka huyu ndiyo wale wanaocheza na watu, wanamuingiza mdomoni bila woga si kwamba anakua ametolewa sumu isipokuwa hana sumu kabisa.

“Mhusika anaweza kukuonyesha umahiri wake wa kucheza naye ukadhani ni mtaalamu wa kucheza na nyoka kumbe hana sumu ndiyo maana wanamtumia kwenye maonyesho,” anasema.

Pia kuna jamii nyingine ya nyoka anayeitwa ‘green mamba’ nyoka wa aina hii wanatajwa kuwa na sifa ya kupenda umbea.

Nyoka huyu anaelezwa kuwa kupenda maeneo wanayoishi binadamu kwenye miti karibu na makazi ya watu.

“Nyoka huyu anaweza akakaa juu ya mti akisikiliza watu wanavyoongea hapo chini na umbea ukimzidia anaanguka na ukimkanyaga anakung’ata.

“Green mamba akikung’ata sumu yake ikikuingia ukakaa muda wa dakika 30-35 bila kupata matibabu unafariki dunia,” anasema.

Pia kuna nyoka aina ya ‘black mamba’ ambaye anao uwezo wa kikimbia km 84 kwa saa moja.

Hassan anasema nyoka huyo ana uwezo kung’ata kundi la wanyama 150-500 bila kuchoka ndani ya dakika mbili na kuwaachia sumu wote.

“Tabia yake huyu ni akimuona adui anasimama na mkia kisha anang’ata utosini, shingoni na kifuani akilenga kwenye moyo na sumu yake ikifika kwenye moyo inauzima ndani ya dakika tatu,” anasema.

Wako nyoka wengi katika hifadhi hiyo wakiwamo anaconda ambaye anakula mbwa au kuku watano kwa wakati mmoja baada ya hapo chakula kingine atakula baada ya wiki mbili.

Anasema nyoka hawatafuni na katika hali ya kawaida mmemng’enyo wa chakula huanzia mdomoni ambapo unakula chakula, unatafuna, kinapofika tumboni mmeng’enyo unafanya kazi, ndiyo maana binadamu wanaweza kula mara tatu kwa siku.

“Nyoka anapokula kitu anakimeza kama kilivyo kikishafika tumboni kinaoza, siku tatu za mwanzo ni za mmeng’enyo na siku tatu nyingine anapumzika na ndiyo maana  tunawalisha kwa wiki mara moja,” anasema.

Pamoja na mambo mengine, Hassan anazungumzia maisha ya nyoka hao hifadhini hapo  ambayo yanaonekana ni ya kujitenga kuwa ndiyo tabia za nyoka jamii zote yalivyo.

Anasema nyoka hawana maisha ya kifamilia wala kirafiki kama wanyama au ndege ya kukaa pamoja na hii ni kwa sababu hawaaminiani.

“Wako nyoka wanaozaa na wanaotaga, anayetaga mayai akishataga anayaacha mayai kisha yeye huhamia sehemu nyingine huku nyuma mayai hayo yanajiangua yenyewe na watoto hao wanaendelea na maisha yao.

“Pia nyoka hawana mapenzi, jike anapokuwa kwenye joto, dume anajua huyu anataka kupandwa na akishampanda wanaachana na jamii moja inapandana yenyewe kwa yenyewe haziingiliani,” anasema.

Hassan anasema kabla ya dume hajampanda jike, huwa kuna harufu anaisikia na kisha hutokea madume matatu ambayo hushindana kwa kupigana atakayeshinda ndiye anampanda jike huyo.

Anasema jike akishapandwa ile harufu bado inabaki kwa hiyo hukimbilia mbali kujificha ili asipandwe na wengine.

“Kwa kawaida nyoka hufanya mapenzi saa mbili hadi nne na hafanyi tena hadi atage hiyo ni baada ya miezi miwili na hutaga mayai yote kwa wakati mmoja kuanzia 20 na kuendelea.

“Lakini pia umri wa kuishi wa nyoka kitaalamu haupo kutokana na tabia yake ya kujivua gamba, anapojivua gamba anakuwa kama anaanza maisha upya na anaposhindwa kujivua hufa.

“Hatua ngumu ambayo nyoka anapitia ni kujitoa ngozi kwenye maeneo ambayo anajaribu kutoa ngozi katika mazingira ya mawe kama porini ambapo inabidi akae kwenye maji ili ngozi ilainike kisha apite maeneo ambayo yana mawe ili iweze kujitoa anaposhindwa hufariki.

“Kwa hapa kwetu ukiangalia tumewawekea mazingira kama hayo kuna maji, mawe na miti ili kurahisisha hatua hiyo muhimnu kwake,” anasema.

Pamoja na kuwahifadhi nyoka, ndege kama bundi, kanga, bata bukini na wengineo lakini wamewapata wapi hadi kuwahifadhi eneo moja?

Hassan anaeleza: “Hawa nyoka tunawanunua kwa watu, lakini huwezi kununua wala kuuza kama huna kibali kwani serikali imekataza kuuza wala kununua bila kibali, mtu yeyote mwenye kibali cha kukamata nyoka akileta hapa sisi tunanunua.”

Katika hifadhi hiyo wageni wanaotembelea wanatakiwa kulipia Sh 3,000 kwa watu wazima, Sh 1,000 kwa watoto, wageni kutoka nje Sh 10,000 na kutoka Jumuiya Afrika Mashariki (EAC) Sh 3,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles