32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

WAFANYABISHARA VIUMBE PORI HAI KUISHTAKI SERIKALI

01-branch-615

Na HUSSEIN OMAR-DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wa viumbe pori hai nchini, wamepanga kwenda mahakamani kufungua kesi ya madai ya fidia dhidi ya Serikali baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwafungia leseni zao za biashara.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Enock Balilemwa, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya Serikali kushindwa kuwapa majibu ya msingi juu ya kusitishwa kwa leseni zao.

Alisema wamekutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ili kuweza kufahamu hatima ya leseni zao baada ya kushindwa kufikia mwafaka.

“Tumekutana na Waziri leo (juzi), kama mlivyoona wenyewe ameshindwa kutupa majibu sahihi yaliyonyooka, badala yake amekuwa akitudanganya kuwa Serikali ndiyo imezuia leseni zetu wakati si kweli, sasa tumeona sehemu pekee ya kupata haki yetu ni kwenda mahakamani,” alisema Balilemwa.

Alisema watafungua kesi kudai kurudishiwa fedha zao walizolipa kupata leseni za kuzafirishia wanyama hao na kulipwa hasara zote walizoingia katika kipindi chote walichokaa bila kufanya biashara.

Balilemwa alisema kilio chao kinatokana na zuio la Serikali kupitia wizara hiyo, kwamba tangu Machi 17, mwaka huu wamewasababishia hasara ambayo hawawezi kuimudu.

“Januari mwaka huu tulilipa gharama zote na kufuata utaratibu juu ya kupata leseni, lakini ghafla tulipata tangazo kutoka wizarani likitutaka kusitisha kusafirisha wanyama hao.

“Baada ya kuona tangazo hilo, tuliandika barua mbili, moja kwa katibu wa wizara hiyo na nyingine kwa Katibu Ofisi ya Rais kupitia kwa mwanasheria wetu, kuomba kuonana na waziri mwenye dhamana, lakini hatukupewa majibu ya kuridhisha,” alisema Balilemwa.

Alisema kuchukuliwa kwa hatua hiyo, kumewasababishia kuishi maisha magumu kutokana na kusimama kufanya biashara walizokuwa wakizitegemea.

Alisema hali hiyo imesababisha taasisi za kifedha kutaka kuuza mali zao kwa kushindwa kurejesha mikopo waliyokopa.

Mwenyekiti huyo alisema leseni hizo walizoomba na baadaye kusitishwa, ziko za madaraja tofauti yanayoruhusu kukamata viumbe pori hai.

Miongoni mwa viumbe pori walioombewa leseni ni ndege, tumbili, vyura, mijusi, nyoka na wadudu wengineo.

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Waziri Maghembe, alisisitiza msimamo wa Serikali wa kutosafirisha viumbe hao nje ya nchi kwa muda wa miaka mitatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles