RUTH MNKENI NA JAFARI JUMA (TSJ)
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata majambazi wawili wanaodaiwa kuhusika kumuua kwa risasi Mtawa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makoka jijini Dar es Salaam, Cresencia Kapuri (50).
Sista Kapuri ambaye alikuwa mhasibu wa Parokia hiyo, aliuawa Juni 23 mwaka huu mara baada ya kutoka benki kuchukua kiasi cha Sh milioni 20 ambazo ziliporwa na majambazi hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
, alisema majambazi hayo mbali ya kuhusika na mauaji ya mtawa huyo, pia wanahusishwa na tukio la uporaji mali katika Benki ya Barclays Tawi la Kinondoni.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Manase Ogenyeka maarufu kwa jina la Mjeshi (35) mkazi wa Tabata Chang’ombe na Hamisi Shaabani maarufu kama Carlos mkazi wa Magomeni.
Alisema majambazi hao wamekamatwa kutokana na operesheni kali inayoendelea jijini Dar es Salaam baada ya kifo cha mtawa huyo.
“Majambazi hawa wawili hatari licha ya kuhusishwa na kifo cha Mtawa wa Kanisa Katoliki na kupora milioni 20 pia tulikuwa tukiwatafuta kwa muda mrefu kwa tuhuma za tukio la uporaji wa fedha katika Benki ya Barclays Tawi la Kinondoni.
“Jambazi Mjeshi alikuwa akiendesha pikipiki akimbeba jambazi mwenzake akiwa na fuko la mamilioni ya fedha na kutoroka nazo na Carlos ndiye aliyekuwa kiongozi wa tukio hilo,” alisema Kamishna Kova.
Hata hivyo aliendelea kusema kuwa Jeshi la Polisi bado linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wawili waliohusika katika tukio la Sisha.
Aidha alisema mbali na watuhumiwa hao jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata majambazi wengine sita ambao ni Beda Mallya (37) mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Msakuzi, Michael Mushi maarufu Masawe (50) mkazi wa Mbezi Makabe, Sadick Kisia (32) mkazi wa Mbagala Kizuiani, Elibariki Makumba (30) mkazi wa Buguruni Madenge, Nurdini Suleiman (40) mkazi wa Buguruni Madenge na Mrumi Salehe maarufu chai bora (38) mkazi wa Kigogo Fresh.
Alisema watuhumiwa watatu kati ya hao sita ambao ni Makumba, Suleiman na Chai Bora walikamatwa baada ya kutumia hati bandia wakiwa wanaomba kazi ya ulinzi katika Kampuni binafsi ya Instant Security Service iliyopo Mtaa wa Makangira Msasani jijini Dar es Salaam.