Na JUSTIN DAMIAN, MAREKANI
ALIYEKUWA Rais wa Marekani kupitia chama cha Republican, George W Bush, hakupiga kura ya kumchagua Rais yeyote akiwamo mgombea wa chama chake, Donald Trump.
Badala yake, aliwachagua viongozi wengine wa Republican kama maseneta, Jaji. gavana na wagombea wengine wa ngazi za chini.
“Hakupiga kura ya kumchagua Hillary wala Trump, “ msemaji wake, Freddy Ford aliliandikia barua pepe gazeti The Texas Tribune baada ya mtangazaji wa radio moja ya hapa Marekani kutangaza Bush angempigia kura Clinton.
George W. Bush pamoja na baba yake aliyewahi pia kuwa Rais wa Marekani, George H.W Bush walikataa kuridhia uteuzi wa Donald Trump jambo ambalo lilizua minong’ono kuwa huenda wangemuunga mkono Hillary Clinton.
“Hatutatoa maoni yoyote kuhusiana na mbio za urais,” alinukuliwa msemaji wa George H. W. Bush, Jim McGrath
Minong’ono hiyo ilianza Jumatatu jioni baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa binti wa Robert Kennedy, Kathleen Kennedy aliweka picha katika ukurasa wake wa Facebook akiwa na Bush nakuandika, ‘Rais ameniambia atampigia kura Hilllary!’
Katika majibu yake juu ya picha na ujumbe huo, msemaji wa Bush, Jim McGrath hakukataa wala kukubali kama Bush angempigia kura Clinton.
Bada ya taarifa hizo kusambaa zaidi ya Jumanne asubuhi, msemaji huyo aliandika katika akaunti ya Twitter na kuwaonya waandishi wa habari kuacha kuripoti kuhusu Bush kumpigia kura Clinton akisema hakuna anayeweza kuthibitisha kama madai ya Kathleen ni ya kweli
Fununu hizo ziliendelea kusambaa kama moto wa kiangazi baada ya CNN kuripoti kuwa Bush alisema angempigia kura Clinton. CNN walisema ni kweli kuwa Rais huyo mstaafu alimwambia Kathleen Kennedy kuwa angempigia kura Clinton katika hafla moja iliyowakutanisha.
Baadaye msemaji wake huyo aliliandikia gazaeti la Texas Tribune kuwa hakutangaza jambo hilo kwa kundi lolote.