Na Raphael Okello
MKUU wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili amewaweka rumande kwa saa 48, Mkurugenzi  wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka  Bunda (BUWSA), Mansour Mandeba   na Mhandisi Msaidizi, Maisha Marechela, wakidaiwa kushindwa kutoa huduma bora za maji kwa wakazi wa Bunda.
Hao ni maofisa wa kwanza  kuchukuliwa hatua katika mamlaka hiyo baada ya wakazi wa   Bunda kuilalamikia mamlaka hiyo tangu mradi  mkubwa wa maji kuanza mwaka 2006.
Mandeba na Marechela   wamewekwa ndani kwa kudaiwa kushindwa kutekeleza agizo la mkuu huyo wa wilaya tangu  Agosti mwaka huu.
Agizo hilo liliwataka  kutoa maelezo ya kina sababu zilizofanya mradi mkubwa wa maji uliogharimu takriban Sh bilioni tisa  kushindwa kuwapatia maji safi wakazi wa mji huo.
Kabla ya kuwaweka ndani juzi  saa 7.00 mchana,  Bupilipili alidai kuwa watumishi hao ni wahujumu uchumi kwa kuwatoza wateja wa maji tozo zilizo chini ya kiwango kilichoelezwa katika mwongozo wa serikali na
kusababisha mamlaka hiyo kutojiendesha inavyotakiwa.
Alisema suala la kukatika maji kila mara kutokana na uharibifu wa miundombinu ni tatizo sugu linalowatatiza wananchi.
DC alisema mamlaka hiyo ina watumishi wengi wasiokuwa na tija na akashauri wapunguzwe.
Sababu nyingine ni kutoweka wazi kiwango cha adhabu kinachotakiwa kutolewa   na wanaohujumu au kuharibu miundombinu ya maji.