25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

RC akiri kushindwa kusimamia usafi Tanga

Chiku Gallawa
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Kapteni (mstaafu) Chiku Gallawa

Na Amina Omar, Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Kapteni (mstaafu) Chiku Gallawa, amekiri kushindwa kusimamia suala la usafi wa mazingira katika jiji hilo kutokana na kutoungwa mkono na baadhi ya watendaji.

Gallawa aliyasema hayo mbele ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, alipokuwa akikagua mradi wa maji Pongwe nje kidogo ya Jiji la Tanga.

Wananchi wa Jiji la Tanga wana utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi kuanzia saa 2.00 hadi saa 4.30 asubuhi katika mazingira wanamoishi.

Utaratibu huo unasababisha shughuli zote za jamii kusimama kwa muda kupisha kukamilika kazi hiyo.

Hata hivyo, utaratibu huo uliopewa jina la ‘Msaragambo’ unalalamikiwa na wananchi wa Tanga wakidai kuzuiwa kufanya shughuli zote za jamii yakiwamo masoko na maduka ya biashara si sahihi.

Akieleza kilio chake kwa Waziri Ghasia, Kapteni Gallawa alisema ameshindwa kusimamia usafi wa mazingira katika jiji hilo kutokana na baadhi ya watendaji kukingiwa vifua na watendaji wakuu wa TAMISEMI.

Gallawa alisema Jiji la Tanga lilikuwa safi wakati wa aliyekuwa Mkuu Mkuu wa Mkoa huo, Said Kalembo, lakini baada ya kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na yeye, baadhi ya watendaji wamekuwa na kiburi na kukataa kutekeleza majukumu anayowapa ikiwamo kusimamia suala la usafi.

Akijibu malalamiko hayo ya Kapteni Gallawa, Waziri Ghasia alisema wizara hiyo haitamkingia kifua wala kumlinda mtendaji atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake wakati analipwa mshahara unaotokana na kodi za wananchi.

Waziri Ghasia alisema hayuko tayari kuona mtendaji yeyote ndani ya serikali za mitaa ambaye hawajibiki katika majukumu yake huku viongozi wa juu yake wanashindwa kumchukulia hatua za nidhamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles