32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vita ya Simba, Azam na Yanga

yanga-na-simba

NA ZAINAB IDDY

TIMU ya Simba na Azam leo zinachuana vikali katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Yanga wakiwa katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kucheza na Mwadui.

Azam na Simba kila moja zina pointi 10 huku Yanga ikiwa na pointi saba na hiyo itakuwa ni vita ya miamba hiyo ya soka nchini ambao wamekuwa wakitawala ligi.

Azam hivi sasa ipo chini ya kocha Zeben Hernandez, ambapo imecheza mechi nne za ligi na kushinda mechi tatu na sare moja hivyo kujikusanyia pointi 10.

Timu hiyo inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuvunja rekodi kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, baada ya kuvuna pointi sita kwenye michezo yake miwili dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City tangu ilipocheza ligi mwaka 2008.

Kwa upande wa Simba wao wananolewa na kocha Joseph Omog, ambaye aliwahi kuinoa Azam miaka iliyopita pamoja na kuipa ubingwa kwa mara ya kwanza, kabla ya kutimuliwa baada ya kufanya vibaya katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Chini ya Omog, Simba imecheza mechi nne za ligi hadi sasa ambapo imeshinda mara tatu na kutoka sare moja, hivyo kuwa na pointi 10 sawa na Azam lakini wakipishana idadi ya mabao ya kufunga wao wakishika nafasi ya pili.

Kuelekea mchezo huo, Simba itaingia uwanjani ikiwa imetoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Historia inaonyesha kuwa timu hizo zimeshakutana mara 12 na leo ni ya 13 tangu zilipoanza kumenyana kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mara ya kwanza Azam na Simba zimekutana katika mechi ya ligi msimu wa 210/12 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Simba iliifunga Azam mabao 2-1 katika mzunguko wa kwanza na katika mzunguko wa pili walichapwa mabao 3-2 na Azam.

Tangu zilipoanza kukutana Simba inaongoza kwa kushinda mara nne huku Azam ikishinda mechi tatu na kutoka sare mara tano.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, mabingwa watetezi timu ya Yanga  watakuwa ugenini katika Uwanja wa Kambarage, kucheza na Mwadui FC.

Kikosi hicho kitaingia uwanjani kikiwa na wachezaji wake wa kimataifa, Haruna Niyonzima na Vicent Bossou waliokuwa wakizitumikia timu zao za Taifa.

Yanga na Mwadui zilikutana mara ya mwisho msimu uliopita kwenye mzunguko wa kwanza na kutoka sare ya mabao 2-2 katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na katika mzunguko wa pili, Mwadui ilifungwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi nyingine za ligi hiyo leo, Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Mtibwa Sugar wataikaribisha Kagera Sugar katika Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro, wakati Mbao FC wakiwa ugenini katika Uwanja wa Mabatini, Pwani watakapocheza na Ruvu Shooting huku Majimaji wakiwa katika Uwanja wa Majimaji kucheza na Ndanda FC.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa kuchezwa mechi mbili, Stand United wataikaribisha JKT Ruvu katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakati African Lyon watavaana na Toto Africans.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles