27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge atoa Sh milioni 5 za maendeleo

Abdallah UlegaNA GUSTAPHU HAULE, PWANI

MBUNGE wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM), ametoa Sh milioni 5.5 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo katika vijiji vya Kikundi na Mkerezange vilivyopo Kata ya Mkamba.

Miradi inayotekelezwa na fedha hizo ni pamoja na Zahanati ya Kikundi iliyopewa Sh milioni mbili na Kijiji cha Mkerezange kimepata Sh milioni 3.5 zitakazotumika kwa ajili ya kujenga vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi iliyopo kijijini hapo.

Akizungumza katika mkutano wake na wananchi wa Kijiji cha Kikundi, Ulega alisema kazi kubwa kwa sasa ni kutekeleza ilani ya CCM kwa kuwaletea wananchi maendeleo.

“Ndugu zangu, nimekuja hapa kuwashukuru kwa kitendo cha kunipigia kura ili niwe mbunge wenu na leo nasema hamkufanya makosa kunichagua kwani natambua changamoto zilizopo katika Jimbo la Mkuranga.

“Kwa hiyo, naombeni mniamini kama mlivyonipigia kura nami naahidi kuendelea kuwatumikia kadiri nitakavyoweza,” alisema Ulega.

Pamoja na hayo, Ulega alisema ili kufanikisha malengo yake, lazima wananchi washiriki shughuli za maendeleo ili fedha zinazopatikana, ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa.

“Kutokana na jinsi nilivyojipanga, naamini ndani ya miaka mitano ya ubunge wangu, lazima Jimbo la Mkuranga liwe na mabadiliko makubwa tofauti na nilivyolikuta.

“Haiwezekani wananchi waendelee kuteseka kwa kufuata huduma ya afya umbali wa kilomita 10 halafu mbunge yupo, jambo hili siwezi kulivumilia katika jimbo langu.

“Kwa kuwa naguswa na matatizo yenu, nimeamua kuanza kutoa fedha kwa ajili ya kuanza mchakato wa kujenga zahanati katika Kijiji cha Kikundi na ifikapo Desemba mwaka huu, lazima zahanati hiyo iwe imekamilika,” alisema.

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Said Tego, alisema kwa sasa wanapata huduma ya afya katika Kijiji cha Kimazichana kilichopo umbali wa kilomita 10 kutoka kijijini kwao.

Kutokana na umbali huo, alisema wanalazimika kutumia fedha nyingi na kwamba uwepo wa huduma ya afya kijini kwao utawasaidia kupunguza gharama walizokuwa wakizitumia.

Kwa niba ya wananchi wenzake, mwananchi huyo aliahidi kushirikiana na mbunge huyo katika shughuli zote za maendeleo kwa kuwa wana imani naye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles