25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Gari la polisi lachomwa moto

Renata  Mzinga
Renata Mzinga

NA ALLY BADI, LIWALE

GARI la polisi wilayani hapa, limeteketea kwa moto baada ya kuchomwa na wafanyabiashara wa nguo.

Tukio hilo lilitokea juzi saa sita mchaka katika Kijiji cha Litou wakati wafanyabiashara hao walipokuwa wakitoka mnadani katika Kijiji cha Mirui wilayani Liwale wakielekea Nachingwea.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambae hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alilitaja gari hilo la polisi kuwa ni lenye namba za usajili PT 3407 la Kituo cha Polisi Liwale, Mkoa wa Lindi.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wafanyabiashara hao walilichoma gari hilo kwa madai kwamba askari polisi walichelewa kuwaokoa baada ya kutekwa na majambazi.

“Tukio hili limetokea saa 12 jioni katika Kijiji cha Litou likihusisha wafanyabiashara waliokuwa wakitokea  mnadani katika Kijiji cha  Mirui na kuvamiwa  na kundi la  majambazi.

“Taarifa zilizopo ni kwamba, baada kuvamiwa  na  majambazi hao, wafanyabiashara walipambana nao  kwa zaidi ya  saa  mbili na wakati mapambano yakiendelea, baadhi yao walipiga simu polisi kuwajulisha juu ya tukio hilo.

“Jambo la ajabu ni kwamba, pamoja na polisi hao kujulishwa mapema, walichelewa kufika eneo la tukio jambo lililowakera wafanyabiashara hao kwa sababu walikuwa wameshaporwa fedha na mali zao.

“Kwa hiyo, baada ya polisi kufika eneo la tukio wakiwa wamechelewa, waliamua kulichoma moto gari lao kwa lengo la kuonesha hasira zao,” alisema mtoa taarifa huyo.

Pamoja na kuteketeza gari hilo, mtoa taarifa huyo alisema wafanyabiashara hao waliteketeza kwa moto pikipiki moja ya Serikali iliyokuwa ikitumiwa na ofisa elimu, Kata ya Kiangara.

“Hiyo pikipiki ilichomwa moto kwa sababu ni mali ya Serikali ambayo polisi wake walishindwa kuwahi eneo la tukio kuwaokoa,” alisema.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Lindi, Renata  Mzinga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo  na kusema wanaendelea na uchunguzi kabla hawajatoa taarifa zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles