BERN, USWISI
NYOTA anayesumbua kwenye mashindano ya baiskeli nchini Ufaransa kwenye michuano ya Tour de France, Chris Froome, amewapa wasi wasi waandaaji wa michuano hiyo kuwa anatumia madawa, hivyo analazimika kufanyiwa vipimo kila siku.
Froome amekuwa akifanya vizuri kwenye michuano hiyo akiwa na timu yake ya Sky, hivyo tangu ashinde timu hiyo imekuwa ikidhaniwa kuwa inatumia dawa ambazo hazitakiwi michezoni.
Hada sasa idara ambayo inapinga dawa hizo, imekwenda kwenye hoteli iliyopo timu hiyo na tayari wamefanyiwa vipimo mara 13 tangu kuanza kwa michuano hiyo ikiwa sasa ni siku ya 18.
Hata hivyo, Froome ameshangaa kuona wanapimwa mara kwa mara huku zikiwa zimebakia siku tano, ila anaamini kuwa maandalizi yao yanaweza kuwafanya kuwa mabingwa.
Inadaiwa hiyo si mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kudhaniwa kuwa anatumia dawa, aliwahi kudhaniwa mwaka 2013 na 2015 mara baada ya kutwaa ubingwa.
Inasemekana nyota huyo amekuwa akishinda katika mazingira magumu ambayo wenzake wamekuwa wakiyashindwa.
“Hili ni jambo ambalo ninaliona kila wakati nikiwa nawania ubingwa, hata mwaka 2013 na 2015 niliona ninaandamwa sana juu ya vipimo, lakini ukweli utabaki pale pale.
“Kama nilishinda mara zote kwa haki basi ninaamini hata michuano hii timu yangu inaweza kushinda bila wasi wasi kutokana na maandalizi ambayo tumeyafanya.
“Tumebakisha siku tano kumaliza, hivyo tunaamini tunaweza kushangaza watu ambao wanadhana mbaya na sisi,” alisema Froome.