* Wamo wamiliki wa makampuni, wafanyakazi
* Wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo
NA WAANDISHI WETU, DAR/IRINGA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewatia mbaroni wamiliki na wafanyakazi wa kampuni kadhaa zinazodaiwa kukwepa kodi kwa kutengeneza stakabadhi feki.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli, kueleza habari za mfanyabiashara mmoja ambaye amekuwa akifanya miamala ya fedha inayofikia Sh milioni saba hadi nane kwa kila dakika moja na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Pamoja na hatua hiyo, habari zaidi zinaeleza kuwa taasisi hiyo pia imebaini uwepo wa kampuni zaidi ya 300 ambazo zinahusika katika mchezo huo mchafu.
Kampuni hizo zimetakiwa kulipa takribani zaidi ya Sh bilioni 30, ambazo zinaelezwa kuwa zimeibwa kupitia mtindo huo wa kudurufu stakabadhi bandia zenye nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata tangu juzi jioni, zinaeleza kuwa watendaji wa Kampuni ya Farm Plant (T) Limited, wamekamatwa na TAKUKURU kwa uchunguzi zaidi.
“Ni kweli watendaji wa juu wa Farm Plant wamekamatwa na Takukuru, wapo watatu na kwa sasa wamehifadhiwa katika kituo cha Polisi Magomeni kwa uchunguzi zaidi. Na huenda kesho (leo) wakafikishwa mahakamani,” kilisema chanzo chetu cha kuaminika.
MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Benn Lincolin, simu yake iliita bila majibu hadi tunakwenda mitamboni.
Hata hivyo watuhumiwa hao kwa sasa tunawahifadhi majina kutokana na sababu za kitaaluma.
Pamoja na hali hiyo taarifa kutoka mkoani Iringa zinaeleza kuwa Jeshi la Polisi lilimtia mbaroni mmoja wa viongozi wa kampuni iliyotajwa kukwepa kodi na kutengeneza stakabadhi bandia.
Chanzo cha uhakika kililiambia gazeti hili kuwa mfanyabishara huyo alitiwa nguvuni Jumamosi, ambapo jana alisafirishwa hadi jijini Dar es Salaam kuungana na watuhumiwa wengine ambao wote huenda wakafikishwa mahakamani leo.
MTANZANIA ilipomtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna Valentino Mlowola ili kupata ufafanuzi wa kukamatwa kwa watuhumiwa hao, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo hadi atakapopata taarifa kutoka kwa watendaji wake.
“Unajua leo (jana) ni siku ya mapumziko ninachokuomba vuta subira kesho (leo) kwa kuwa ni siku ya kazi njoo ofisini nitakueleza taarifa zote. Maana kuna timu ya watendaji ndiyo wanashughulikia nami nitazungumza hadi pale nitakapopata taarifa hizo,” alisema Kamishna Mlowola.
Wiki iliyopita wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mlowola pamoja na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, walieleza jinsi kampuni hizo feki zilivyoiibia Serikali kupitia stakabadhi za mfumo wa kielektroniki (EFD’s).
Kamishna Kidata, alisema kampuni hizo zimekuwa zikinunua stakabadhi za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za kielektroniki ambazo hazijasajiliwa na kuzitumia na kisha kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwapo na bidhaa au stakabadhi halali iliyouzwa au kutolewa na muhusika.
Alisema TRA kwa kushirikiana na Takukuru bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kampuni zote zinazojihusisha na mchezo huo mchafu wa kuiibia Serikali.
Mtendaji huyo wa TRA alisema hadi sasa tayari wamezibaini kampuni nne ambazo zimekuwa zikijihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huo tangu mwaka 2010 hadi 2014 na kupoteza mapato ya Serikali kiasi cha Sh bilioni 29.2.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Skol Building Material Ltd, ambayo imebainika tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa VAT ya Sh bilioni 5.4 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh bilioni 10.9, hivyo kudaiwa jumla ya Sh bilioni 16 kwa kipindi hicho.
Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Ltd, ambayo alisema tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikuwahi kulipa VAT ya jumla ya Sh bilioni 5 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh bilioni 4 ambayo ni jumla ya kodi inayodaiwa kufikia Sh bilioni 9.
“Kampuni nyingine ni A. M Trailer Manufacturers Ltd ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014 haikuwahi kulipa VAT ya Sh bilioni 6 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh bilioni 1 ambayo jumla ya fedha inazotakiwa kurejesha ni Sh bilioni 1.7.
“Baada ya kubaini ukwepaji kodi wa makampuni haya, TRA kwa kushirikiana na Takukuru inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na baada ya uchunguzi kukamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwepa kodi,’’ alisema Kidata.
Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa wafanyabiashara kutojihusisha na kununua stakabadhi bandia, na kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa mamlaka imejizatiti kuendelea kuwabaini wakwepa kodi wote.
Kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa TRA kujihusisha na mtandao huo wa kudurufu mfumo wa kukwepa kodi na kuiibia Serikali, alisema wanaendelea na uchunguzi na kama wapo nao watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Kamishna Mlowola, alisema uchunguzi bado unaendela kwa kampuni 300 ambazo zimetakiwa kulipa fedha hizo na wakishindwa watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Pamoja na hali hiyo, alisema mfanyabiashara huyo aliyebainika kuwa na makampuni mengi, alikuwa akishirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) pamoja na TRA.
Mtandao mpana
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa mtandao wa wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakiibia Serikali, upo kwa makampuni zaidi ya 20,000 ambazo zimekuwa zikiendesha mchezo huo mchafu tangu 2010.
Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa kwa wiki moja sasa vyombo vya dola vimekuwa vikipambana na mtandao huo ambapo inaelezwa kuwa vinara hao tayari wapo katika mikono salama.