NA MARTIN MAZUGWA, DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyakazi wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, Dar es Salaam, waliokuwa wameitisha mgomo wakitaka menejimenti ya kiwanda hicho iwalipe stahili zao.
Polisi wa Kituo cha Urafiki walijaribu kuwatuliza wafanyakazi hao bila mafanikio ndipo walipolazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyakazi hao waliokuwa wakiwashambulia polisi kwa mawe.
Habari zinasema vurugu hizo zilizuka baada ya pande mbili kushindwa kuafikiana kuhusu malipo ya malimbikizo na madeni ya wafanyakazi yanayofikia Sh bilioni 9.5 huku uongozi wa kiwanda ukidai hauna uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha.
Katika vurugu hizo watu watatu walipoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Palestina, Sinza huku mtu mmoja akishikiliwa na polisi akidaiwa kumpiga na kumnyang’anya simu mwanamke katika vurugu hizo.
Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Hassani Mwanji,aliliambia MTANZANIA kuwa madai yao yalitakiwa kuwa yametekelezwa Aprili 30 mwaka huu kama mahakama ilivyokuwa imeamua, lakini wanashangaa hadi sasa hawajalipwa fedha zao kitu kinachosababisha washindwe kufanyakazi.
“Tunashindwa kuelewa uongozi wa Kiwanda cha Urafiki kushindwa kutimiza maagizo ya mahakama kutupatia haki yetu, tumechoshwa na ahadi zao , tunataka haki yetu,” alisema mfanyakazi huyo.
Naye Meneja Rasilimali watu wa kiwanda hicho, Dicksoni Machilila, alisema kiwanda hakina uwezo wa kulipa deni hilo kutokana na kushuka uzalishaji.
Alisema kwa sababu hiyo hivi sasa kinafanya kazi kwa zamu moja badala ya tatu zilizokuwapo awali.
“Kiwanda hakijakataa kulipa madeni yao kama Mahakama ilivyoagiza kwamba tulitakiwa kulipa fedha hizo Aprili 30 lakini itakuwa haitawezekana kutokana na kushuka uzalishaji wa kiwanda,” alisema.
Alisema Watanzania wana asilimia 49 katika kiwanda hicho, huku mwekezaji (Mchina) akimiliki asilimia 51 kwa sababu hiyo mamlaka ya uamuzi wowote yako mikononi mwa Wachina.