Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Chama cha Tanzania Labour (TLP) kimesema kitahakikisha kinawanadi wagombea wake zaidi ya 180 wanaoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa wanaamini wote wana uwezo na watashinda.
Akizungumza Novemba 21,2024 wakati wa kampeni zilizofanyika katika Mtaa wa Makuti A Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lyimo, amesema
“Chama chetu hakina uwwezo lakini tunaendelea kupambana kuhakikisha wagombea wetu wanaopeperusha bendera ya TLP tunawanadi wote. Jana (Novemba 20,2024) tulizindua kampeni katika Mkoa wa Kilimanjaro na kesho (Novemba 22,2024) tutazindua Mwanza…wagombea wengi tuliowaweka wana uwezo na tunaamini tutashinda viti vingi,” amesema Lyimo.
Amewashauri wananchi kuwachagua wagombea wana shughuli za kufanya kuepuka vitendo vya kupokea rushwa alivyodai kuwa vimekuwa vikifanywa na viongozi wasiokuwa na kazi za kuwaingizia kipato na kutumia nafasi zao vibaya.
“Kiongozi wa mtaa anatakiwa awe na shughuli ya kufanya asiwe na njaa, akiwa na njaaa maana yake yuko tayari kununuliwa kwahiyo anaweza kupokea rushwa. Tunawashauri kinamama wawaunge mkono wagombea wetu wanawake ambao tumewasimamisha maeneo mengi, waoneshe mfano kwa sababu hata rais tuliyenaye na mwanamama,” amesema.
Naye mgombea Uenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makuti A, Stella Mrema, amesema
iwapo atachaguliwa atahakikisha huduma za barua za utambulisho zitatolewa bure katika mtaa huo.
Amesema wananchi wamekuwa wakitozwa kati ya Sh 2,000 hadi Sh 5,000 pindi wanapohitaji barua za utambulisho kwa ajili ya kwenda kuwadhamini ndugu zao au kupeleka kwenye taasisi mbalimbali.
“Mkinichagua nitahakikisha huduma za barua za utambulisho zitatolewa bure pamoja na kushughulikia barabara ya mtaa wetu anbayo ni mbovu, mvua zikinyesha wananchi wanazibua vyoo hivyo nitatahakikisha nalifanyia kazi,”amesema Stella.
Pia amesema atashughulikia upatikanaji wa mikopo kwa wanawake na vijana ili kuhakikisha wanajikomboa kiuchumi