IDARA ya Uhamiaji mkoani Tanga imewakamata wahamiaji haramu 177 walioingia nchini bila vibali.
Kati ya raia hao wa mataifa mbalimbali 22, walikamatwa kwa kufanya kazi bila kibali kwenye taasisi, mashirika na kampuni za mkoani hapa.
Akizungumza katika mahojiano na MTANZANIA Jumamosi jana, Kaimu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga, Deodat Bazil, alisema wapo raia sita wa Tanzania wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na usafirishaji wa wahamiaji hao.
Aliwataja raia waliokamatwa kwa kosa la kufanya kazi mkoani humo bila vibali kuwa ni kutoka nchi za Kenya, Ufaransa, Ghana, China, Uholanzi, India, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Ethiopia.
“Watuhumiwa hao walikamatwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu. Kesi zao zipo mahakamani zinaendelea kutokana na tuhuma zinazowakabili ambazo ni uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema Bazil.
Alisema nchi inayoongoza kwa raia wake kuingia nchini bila vibali halali ni Ethiopia na katika kipindi cha miezi mitatu kumekuwa na ongezeko la raia wengine kutoka Somalia, Korea Kusini, Burundi na China.
Aliomba ushirikiano kwa wananchi ili kuwafichua wahamiaji haramu waliopo katika maeneo yao ikiwa ni hatua mojawapo ya kuimarisha hali ya ulinzi na usalama wa raia.