Na Mwandishi wetu, Arusha
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Umma,Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) wamekutana katika kikao maalumu kwa siku mbili jijini Arusha wakijadili mambo mbalimbali.
Kikao hicho kimefanyika kuanzia Aprili 4 – 5, 2024 ambapo wamepitia pia Sera za Shimmuta (Shimmuta Policy), Mpango Mkakati ya Shimmuta, tathmini ya mashindano yaliyofanyika mwaka 2023 jijini Dodoma.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) na kufunguliwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof.Epaphra Manamba.
Mbali na hayo wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na wajumbe wameendelea kumpongeza Makamu wa Rais Philip I.Mpango ambaye ndiye mlezi wa shirikisho hilo kwa kuendelea kuwapa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha mafanikio ya shirikisho yanaonekana.
Mwenyekiti wa SHIMMUTA,Roselyn Massam amesema Shirikisho linatamani na linafanya juhudi kubwa kuhakikisha linafikia malengo ya kuwa na mashirika wanachama mengi ili kutekeleza sera ya michezo mahala pa kazi ambayo imekuwa chachu kubwa katika kuwaweka wafanyakazi pamoja na kuwaongezea morali ya utendaji kazi.
Mbali na hilo Kamati ya Utendaji ya Shirikisho imeeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika muda mfupi toka uongozi huo uingie madarakani ikiwemo kuongeza wanachama na ushiriki wa wanachama kuwa mkubwa zaidi mfano mwaka 2023 zaidi ya Mashirika, Taasisi na Makampuni 50 yalishiriki.
Wajumbe wa mkutano wameadhimia kwenda kufanyia utekelezaji yale yote yaliyojadiliwa katika mkutano huo.