Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kushiriki katika maamuzi yanayohusu masuala ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo utoaji wa maoni kuhusu marekebisho ya sera mpya ya mambo ya nje ya mwaka 2001.
Hayo ameyasema Januari 9, 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba wakati akifungua kongamano la kukusanya maoni ya wadau mahsusi kuhusu mapendekezo na marekebisho ya sera mpya ya mambo ya nje ya mwaka 2001 lilofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Julias Nyerere (JNCC).
Amesema kuna umuhimu wa wadau mbalimbali kushirikishwa kutoa maoni yao mahsusi katika mchakato wa marekebisho ya sera mpya ya mambo ya nje ya mwaka 2001.
“Tanzania kama yalivyomataifa mengine, ambayo nchi zao zinavyokabiliwa na fursa na changamoto katika ushiriki wake kwenye jukwaa ya kimataifa. Ni vema kuwa na sera madhubuti ambayo ni muhimu katika kutumia ipasavyo fursa hizo na kukabiliana na changamoto ambazo zitajitokeza.Kuna umuhimu wa maoni mbalimbali yanayotolewa na wadau katika kuwezesha uwepo wa sera yenye tija ,itakayokidhi matarajio ya wananchi,” amesema Makamba.
Amesema kuna umuhimu wa kupata maoni ya sera hiyo ili kuwezesha taifa kunufaika ipasavyo na fursa zitokanazo na ushirikiano wa kikanda na kimataifa hasa utekelezaji wa dhana ya diplomasia ya uchumi.
Aidha, amesema ndani ya kongamano hilo wadau hao watapata fursa adhim ya kuelewa kwa kina masuala muhimu yaliyomo katika sera ya mambo ya nje ikiwemo misingi ya sera zao na malengo yake.
”Wataweza kupata uelewa wa historia ya sera ya mambo ya nje tangu uhuru hadi 2001 ambapo utekelezaji wa sera kuanzia mwaka 2001 hadi sasa mapitio ya sera hiyo,” amesema.
Amesema katika kongamano hilo,wizara yake inapenda kusikia kutoka kwa wadau jinsi wanavyoona marekebisho yaliyofanyika katika sera na ni maoni gani waliokuwa nayo kuhusu njia zitakazochukuliwa kufikia malengo wanayotamani kufikia.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassoro amesema sera ya Mambo ya Nje ni misingi ya uhusiano wa Nchi na Mataifa mengine,hivyo iliunda timu ya pamoja ya wataalam na kufanya tathmini ya mapitio ya sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 ili kufanya marekebisho yatayoendana na mahitaji ya sasa.
Amesema zoezi hilo la tathmini na mapitio limetumia mbinu mbalimbali ikiwemo mahojiano na wadau na kufanya tafiti katika vyombo vya habari mbalimbali kusambaza madodoso katika muendelezo huo wanakusanya maoni kupitia kongamano hilo.
Baadhi ya wadau wa kongamano hilo, akiwemo Mwanasiasa mkongwe Profesa Anna Tibaijuka, amependekeza kuwepo na timu ya wataalamu wa kidiplomasia kwamba waheshimike katika kufanya utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo maboresho ya sera hiyo.
Profesa Tibaijuka amesema wataalamu hao endapo wataheshimiwa na kuthaminiwa wataweza kusaidia kutumiwa katika maeneo mbalimbali kwani wataweza kukuza uchumi wa kidipromasia ndani na Nje ya Nchi.
Kwa upande wake Mwanasiasa mkongwe na Mbobezi wa masuala ya Uchumi, Profess Ibrahim Lipumba ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha wanafanya mchakato wa kuwaandaa vijana wa Sasa na wa baadaye kuwa wanadipromasia wapya na mahiri watakaoweza kuimarisha hali ya kisiasa na kiuchumi ndani na Nje ya Nchi.