Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Kampuni ya Lake Energies kwa kushirikiana na Vodacom wameunga mkono watachangia juhudi za Serikali za kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali kwa kuwahamasisha watanzania kuachana kubeba fedha taslimu badala yake watumie mifumo ya kidigitali kufanya malipo.
Hayo amebainishwa leo Desemba 20,2023, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Operesheni za M-pesa Vodacom, Titi Mbise wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema mkakati wao nj kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidigitali kuhakikisha kunakuwa na usalama,urahisi katika shughuli za biashara.
Amesema ushirikiano huo unawafanya wateja wote wa Lake Energies kulipia huduma kwa simu ya mkononi kupitia M-pesa katika vituo vyote vya mafuta nchi nzima.
“Kupitia ushirikiano huu ni kurahisisha malipo ya wateja asilimia 10 ya malipo yao ya mafuta wanapofanya malipo kupitia M-pesa siku za Ijumaa na Jumapili kuanzia msimu wa sikukuu hadi Januari mwakani.
Tunaelewa watu wengi wanasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kuwatembelea wapendwa wao wakati huu, suluhisho la malipo ni kidigitali,”amesema Mbise.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Huduma za Rejareja wa Lake Energies nchini, Fredy Mchau amesema dhamira yao ni kuhakikisha wateja wanaotembelea vituo vyao wanapata huduma mbalimbali za malipo.
“Ushirikiano huu na kampuni inayojitolea kutoa suluhisho za malipo kidigitali ni hatua muhimu kuelekea katika lengo hili na huduma zinapatikana Lake Energies katika vituo 139 nchini kote,”amesema Mchau.