WASICHANA wenye uwezo wa kuigiza wametakiwa kuchangamkia fursa kwa kujitokeza kwa wingi katika usaili wa filamu mpya ya ‘XBaller’, utakaofanyika kesho katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa usaili huo ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Marekani, Ernest Napoleon, alisema usaili huo utaanza saa 5:00 asubuhi.
Ernest, ambaye pia ni mshindi wa filamu bora East Africa katika tuzo za Filamu za Kimataifa kwa nchi za Jahazi (ZIFF) kupitia filamu yake ya Going Bongo, alifafanua kwamba watakaopata nafasi ya kusailiwa ni wasichana wenye umri kati ya miaka 16 na 30 na watakaoshinda watapata fursa mbalimbali, ikiwemo kuigiza na wasanii wengine kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Uingereza.
“Kwa sasa tunafanya kwa ajili ya wasichana tu na tutakaporudi tena tutafanya kwa ajili ya wanaume, hivyo wasichana wenye vipaji vya kuigiza wajitokeze kwa wingi kutumia fursa hii maana filamu ya ‘XBaller’ itashirikisha waigizaji kutoka nchi mbalimbali wa ndani na nje,’’ alisema Napoleon.
Hata hivyo, washiriki wote wametakiwa kutembelea mtandao wa http://bit.ly/xballerauditionsdar ili kupata mwongozo wa miswada (Script) ya kuwaongoza katika zoezi hilo la usaili. Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa, Dimba na The African ni mmoja wa wadhamini.