25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JK, Ukawa wakubaliana

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TDC) alipokutana nao jana Ikulu ndogo mjini Dodoma. Picha na Ikulu
Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TDC) alipokutana nao jana Ikulu ndogo mjini Dodoma. Picha na Ikulu

NA WAANDISHI WETU DAR, DODOMA

HATIMAYE mvutano kati ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Serikali umefikia kikomo baada ya pande mbili hizo kukubaliana na Rais Jakaya Kikwete kuboresha Katiba ya mwaka 1977 na kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani.

Hatima hiyo ilifikiwa jana kwenye kikao kilichofanyika kati ya Rais Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinachoundwa na vyama vyenye wabunge ambavyo ni CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, TLP, UDP na UPDP inayowakilisha vyama visivyo wa wabunge, kilichofanyika Ikulu ndogo mjini Dodoma.

Mkutano wa awali wa viongozi hao ulifanyika Agosti 31, mwaka huu, katika Ikulu ya Kilimani, mjini Dodoma ambapo walipeana majukumu ya kufanya ili kuangalia namna bora ya kufikia mwafaka.

Katika mkutano wa jana, chanzo cha habari kutoka ndani ya mkutano huo kilieleza kuwa viongozi hao walikubaliana kuwa kutokana na mazingira ya sasa, ni vigumu kupata Katiba mpya ambayo itatumika mwakani.

Kutokana na hali hiyo, viongozi hao walikubaliana kuwa ni vyema vyama hivyo vikakaa na kuangalia mambo muhimu ya kuwekwa kwenye Katiba ya sasa.

“Vyama vinatakiwa vikae na kuangalia ni nini cha kuchukuliwa na kuwekwa kwenye Katiba hii ya sasa, baada ya kumaliza Uchaguzi Mkuu ndiyo sasa turudi kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya,” alisema.

Alisema kuwa baada ya vyama hivyo kukaa na kukubaliana kitu cha kuweka kwenye Katiba inayotumika sasa, watayapeleka mapendekezo hayo serikalini kisha muswada wa marekebisho ya Katiba utapelekwa bungeni.

Kwenye suala la kuahirishwa kwa Bunge, chanzo kingine kilisema kuwa halikuzungumziwa, lakini busara inatarajiwa kutumika zaidi.

Mwenyekiti TCD

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, alisema kuwa wamekubaliana kindugu.

Waandishi wa habari walipotaka afafanue kauli yake na kama kukubaliana huko kunamaanisha kusitisha Bunge ama Ukawa kurudi bungeni, Cheyo alisema: “Mimi naongea kama mwenyekiti wa vyama vyote, tumekubaliana kindugu, mazungumzo yalienda vizuri na kesho nitatoa taarifa kamili.”

Mwanasheria Mkuu

Agosti 16, mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, alizungumzia ugumu wa rais kuvunja Bunge la Katiba na kusema Katiba mpya ikishindwa kupatikana, iliyopo sasa itafanyiwa marekebisho.

Jaji Werema alikuwa akizungumzia hatima ya upatikanaji wa Katiba mpya na mwenendo wa vikao vya kamati za Bunge Maalumu vinavyoendelea sasa Dodoma, ambavyo vimesusiwa na wajumbe wanaounda Ukawa.

Alisema tathmini iliyofanyika ya mwenendo wa vikao hivyo, imeonyesha kuwa theluthi mbili inayohitajika ili kupitisha vifungu vinavyojadiliwa inapatikana, isipokuwa wasiwasi umebaki kwenye kupitisha vifungu hivyo wakati wa vikao vya pamoja vya wabunge wote.

Jaji Werema alisema kwa kutambua hilo, iwapo akidi ya theluthi mbili ya wajumbe haitapatikana wakati wa kupitisha Katiba iliyopendekezwa, baadhi ya vifungu vitakavyopitishwa vitachukuliwa na kupelekwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kuingizwa kwenye Katiba ya sasa ya mwaka 1977.

“Kwa sasa akidi kwenye kamati inatosha, tukifikia Bunge kuja na Katiba inayopendekezwa na kama hakuna theluthi mbili, tutarudi kwenye Bunge la kawaida (Bunge la Jamhuri ya Muungano) na kukubaliana, yaliyokuwa hayana ubishi tutayaweka na kuyatumia kwenye Katiba ya sasa, likiwamo suala la mgombea binafsi,” alisema Jaji Werema.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles