27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kipunguni waiomba Serikali kuharakisha malipo yao

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakazi 1,865 wa Mtaa wa Kipunguni ambao wanatakiwa kuhama kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wameiomba Serikali kuharakisha ulipaji fidia.

Julai 7,2023 Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, aliwahakikishia wakazi hao kuwa watalipwa fidia kabla ya Oktoba 2023 kwa kuwa fedha zipo lakini mpaka sasa hawajalipwa.

Wakizungumza Novemba 15,2023 wakati wa mkutano wa hadhara wakazi hao wamesema tangu ahadi hiyo itolewe utekelezaji bado haujafanyika.

“Tulifanyiwa tathmini tangu mwezi wa saba mwaka jana lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea, hali yetu inazidi kuwa ngumu, tulikuwa na nyumba za wapangaji lakini wengi wameondoka.

“Taarifa tunazopewa kwamba tunashindwa kulipwa kwa sababu kuna migogoro baina yetu sio kweli, hakuna mwananchi aliyekataa kusaini malipo kwa sababu fedha ndogo…wote tunasubiri tupewe haki zetu tuondoke,” amesema mmoja wa wakazi hao, Beatrice Kimanga.

Mkazi mwingine wa Kipunguni Aseri Anaeli, amesema wamesubiri fidia kwa muda mrefu hali iliyosababisha washinde kuendeleza makazi yao.

“Tuliahidiwa baada ya mwezi wa tisa tutaondoka lakini mpaka sasa hakuna kinachoeleweka, ambao hatuna matatizo ni wengi kwa nini tusilipwe?

“Namuomba mama yetu Rais Samia atusikilize wananchi wa Kipunguni tunateseka, hatujui kesho yetu, usalama wa maisha yetu umekuwa mdogo,” amesema Anaeli.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipunguni, Mwinjuma Seke, amesema kwa sasa hakuna tena mgogoro bali wananchi wanasubiri walipwe fidia waondoke.

“Hatuna mgogoro wa viwanja, hakuna mwananchi aliyefanyiwa tathmini anayepinga malipo kwahiyo tunasubiri malipo,” amesema Seke.

Amesema pia waliozika ndugu zao katika mtaa huo wajitokeze ili waweze kulipwa na kuhamisha makaburi.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amewataka wakazi hao kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kurahisisha zoezi la ulipaji fidia.

“Wakati nazungumza bungeni mheshimiwa Waziri (Dk. Nchemba) alisema watu waliopewa viwanja ndio wanawachelewesha, tumeandikiwa barua tufanye huu mkutano ili waanze kulipa.

“Kwahiyo waliopewa viwanja waseme kama wanavikubali na ambao hawavitaki, wenye viwanja lakini wameshaviendeleza waseme ili TAA (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege) ipate orodha kamili, hakuna fedha ya serikali ambayo inalipwa bila kuwa na takwimu sahihi,” amesema Bonnah.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles