Na Derick Milton, Bunda
KUTOKANA na uwepo wa Changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imewasisitiza wakulima wa zao la mpunga kutumia teknolojia ya kilimo shadidi kwenye zao hilo ili kukabiliana hali hiyo na kuzalisha kwa tija.
Akizungumza na wakulima pamoja na maofisa ugani katika skimu ya umwagiliaji ya Maliwanda, wilayani Bunda mkoani Mara, Mtafiti Uchumi na Jinsia kutoka TARI Dk.Theodore Kessy amesema ili wakulima wa zao la mpunga waweze kukabiliana na changamoto hiyo wanashauriwa kutumia teknolojia ya kilimo shadidi.
Dk. Kessy amesema kilimo shadidi kwenye zao la mpunga ni teknolojia ambayo miche michanga yenye umri kuanzia siku 8 hadi 14, hupandikizwa mche mmoja kwenye shimo, kwa nafasi pana sentimeta 25 kwa 25 na mkulima utakiwa kufanya palizi kwa kutumia vipalizi umwagiliaji wa kulowesha na kukausha shambaa kuweka mbolea.
Amesema teknolojia hiyo ni muhimu kwani mkulima analazimika kulima eneo dogo lakini ana uwezo wa kuvuna mazao mengi ikiwa atafuata kanuni zote zinazotakiwa ambapo hekari moja anaweza vuna wastani wa hadi 10 za mpunga.
Naye mtafiti na mgunduzi kutoka TARI, Dk. Juliana Mwakasendo amebainisha kuwa teknolojia ya kilimo shadidi ni tofauti a kilimo cha kawaida, kwani hakihitaji maji mengi, ambapo mkulima atatakiwa kuweka maji kwenye shamba lake pale itakapohitajika.
” Tunajua kwenye kilimo cha kawaida cha zao hili wakulima hugombania hadi maji maana kila mmoja anahitaji, lakini kilimo shadidi mkulima anahitaji maji kidogo, maji yanawekwa kwenye shamba pindi tu yanapokauka ndipo mkulima anatakiwa kuweka mengine, siyo kila wakati shamba limejaa maji,” ameeleza Dk. Mwakasendo.
Amewashauri wakulima wa zao hilo nchini kubadilika na kuona kama ni zao la kibiashara kwa kuacha kulima kwa mazoea, huku akisisitiza matumizi ya teknolojia hiyo kuwa tasaidia kuzalisha kwa tija na uwepo wa uhakika wa chakula.
TARI inatekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wakulima na maofisa ugani juu ya teknolojia ya kilimo shadidi kwenye zao la mpunga kupitia vituo vyake vya Uyole, Ifakara na Mikocheni katika Wilaya za Mbarali, Iringa vijijini, Bunda vijijini, Kilombero na Pwani.
Mradi huo unaofadhiliwa na ‘Norwegian Agency for Development Cooperation’ unalenga kuwajengea uwezo wa kitaasisi juu ya mifumo ya uzalishaji wa zao la mpunga inayokuabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na rasilimali kwa ufanisi kwa kuzingatia kilimo shadidi.