Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Jumla ya klabu 14 za mchezo wa kuogelea zinatarajia kuchuana katika mashindano ya Taifa yatakayofanyika Septemba 23-24, 2023, kwenye bwawa la shule ya Kimataifa Tanganyika, Masaki, jijini Dar es Salaam.
Klabu hizo zitakazoshiriki zinatoka mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Arusha, Morogoro, Dar es Salaam na Zanzibar.
Akizungumzia mashindano hayo, Mratibu wa Habari wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA) Sebastian Kolwowa, amesema licha ya kuwa mashindano ya wazi lakini wanaoruhusiwa kushiriki ni waogeleaji wanachama wao.
Amesema utofauti wa mashindano hayo pamoja na kurudisha klabu, kila mchezaji ataogelea kivyake na zawadi zitatolewa kwa muogeleaji mmoja mmoja.
“Tunawakaribisha watu wote wanaopenda kuja kutazama mashindano, ni bure hakuna kiingilio chochote,” ameeleza Kolwowa.