Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini wameomba kukutana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ili kujadili silabasi ya masomo ya dini ya kiislam kujenge mustakabali mwema wa Taifa.
Akizumgumza leo Agosti 10, jiji Dar es Salaam na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhajj Sheikh Musa Kundecha amesema kipindi cha nyuma ilikubali masomo ya dini yataandaliwa kwa pamoja baina ya wanadini na Serikali.
Amesema kupatikana kwa silabasi na vitabu kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vya ualimu yataandaliwa wanadini na serikali kwa pamoja.
“Kwa kuwa tumemuandikia barua waziri mwenye dhamana tunaomba akutane nasi ili kujenga mustakabali mwema wa nchi yetu na kujadili silabasi hizi,” amesema Alhajj Sheikh Kundecha.
Aidha, amesema wamepokea kwa masikitiko serikali imeshaanda tayari silabasi (mihutasari) za masomo ya dini na kuondoa mambo yote ya imani ya dini hizo.
Naye Sheikh Issa Ponda amesema wana mtaala wao na ni chombo ambacho kinatambulika na serikali na kipo kisheria.
“Viongozi wenye dhamana ya elimu watuite watushirikishe juu ya mtaala wao tujadiliane kwa pamoja watuambie nini kinahitajika ili tupate mustakabali, “amesema Sheikh Ponda.