30.4 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanza yaadhimisha miaka 59 ya Muungano kwa kuzindua kampeni ya uhifadhi mazingira na chanjo

Na Clara Matimo, Mwanza

Mkoa wa Mwanza leo Aprili 26,2023 umeadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuzindua kampeni ya kupanda miti milioni 23 na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo dhidi ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika kimkoa Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza kwenye viwanja vya Chuo cha Ufundi Stadi(VETA) kilichopo wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema lengo ni kukabiliana na changamoto ya ukame na mabadiliko ya tabia nchi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa(MNEC), Jamal Abdul Babu akipanda mti katika eneo la Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza kwenye maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lengo likiwa ni kutunza na kuhifadhi mazingira.

Amesema mkoa huo umedhamiria kuwa wa mfano kitaifa kwa kupanda na kutunza miti pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji ambapo wataweka mikakati ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa mzalendo katika kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira.

“Leo tumezindua kampeni hii kwa kupanda miti 1,270 katika eneo hili la chuo cha veta nakuagiza Mkuu wa chuo hiki pamoja na viongozi wa kijiji na Kata hakikisheni mnaitunza ili ikue, tutatengeneza elimu chungu kwa wananchi ili watunze mazingira tunachohitaji ni kukabiliana na ukame pamoja na mabadiliko ya tabianchi wote tuwe na moyo wa kuijenga Tanzania yetu kwa faida yetu na vizazi vijavyo,” amesema Malima na kuongeza:

“Kila eneo litakalopandwa miti Mwenyekiti na Mtendaji wa Kijiji watawajibika kuilinda hatuwezi kuwa tunafanya mchezo kwenye mambo ya muhimu, kama mwananchi atapeleka mifugo yake kuchunga kwenye eneo lililopandwa miti atalipa faini pamoja na kupanda miti iliyoliwa ama kuharibiwa na mifugo wake,” amesema.

Ameongeza kwamba ili kufanikisha lengo hilo la kupanda miti milioni 23, kila wilaya zimepangiwa kiasi cha miti ya kupanda ambapo amefafanua kwamba Wilaya za Ilemela na Nyamagana kwa kuwa hazina maeneo ya kupanda miti zitalazimika kununua maeneo kwenye wilaya zingine mkoani humo na kupanda miti hiyo kisha zitaimiliki.

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kimkoa Eilaya ya Kwimba mkoani humo.

Akizungumzia umuhimu wa chanjo za polio, surua, kifua kikuu na homa ya ini kwa watoto wenye umri chini ya miaka miwili Malima amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kuandaa elimu watakayowapa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo kwa kundi hilo ili kuwaepusha na madhira mbalimbali yanayoweza kuwapata ikiwemo vifo au ulemavu.

“Hakuna uhalali wa mama au mzazi kutompeleka kliniki mtoto wake kupata chanjo wakati serikali inazitoa bure ili kulinda afya za watoto wake ambao ndiyo taifa la kesho,” amesema Malima.

Awaasa wananchi kuhusu Muungano

Akizungumzia namna ya kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na viongozi wa nchi hizo Aprili 26, 1964 Mkuu huyo wa Mkoa Malima amewataka wananchi wa mkoa huo kuvumiliana, kustahimiliana, kuheshimiana, kupendana, kusaidiana na kukosoana wakiambiana ukweli kwa staha maana ni jambo jema lakini si kwa kutukanana.

“Tuuenzi muungano wetu na kuwaenzi viongozi wetu waliouasissi muungano huo kwa kufuata hayo niliyoyasema maana tukiyafuata hayo tutaendelea kudumisha amani yetu iliyopo nchini ambayo ndiyo mtaji mkubwa wa maendeleo ya taifa, jamii, familia na mtu mmoja mmoja, ukimuona mtu anaubeza muungano ujue hajitambui na ni mtu hatari katika muungano.

“Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2023 inasema ‘Umoja na Mshikamano ndiyo nguzo ya kukuza uchumi wetu’hivyo tushikamane katika kuhakikishe tunakataa mambo ambayo si maadili ya watanzania tuheshimu maadili yetu, tutumie maadhimisho haya ya miaka 59 ya muungano wetu kuwaombea viongozi wetu waasisi wa muungano pamoja na viongozi wa chama tawala CCM na wale wa serikali ili waendelee kutuongoza kwa haki na waasisi wetu Mwenyezi Mungu awape pumziko jema,” amesema Malima.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa (MNEC), jamal Abdul Babu akizungumza kwenye maadhimisho hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Mwanza Sixbert Jichabu, amewaasa wananchi kuuenzi muungano kwa kuwa na nidhamu pia uadilifu kwani ndiyo silaha ya ushindi kwa kila jambo.

“Leo tumepanda miti na kuzindua kampeni ya kupanda miti milioni 23, ili tuweze kutimiza lengo hilo kila mtu awe mzalendo kwa kushiriki katika kuitunza huo ndiyo utanzania maana waasisi waliujenga muungano huu katika misingi thabiti ya uzalendo,” amesema MNEC huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles