Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa Serikali imefikia uamuzi wake wa kuingia makubaliano na kampuni zenye uwezo wa kuchimba na kuchakata madini nchini ili nchi iweze kunufaika na kupata faida kutokana na raslimali hizo kwa kuunda kampuni za ubia na hivyo Serikali kunufaika kupitia tozo, kodi, ajira, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa teknolojia.
Amesema hayo leo Aprili 17, 2023 Chamwino Ikulu Dodoma wakati akishuhudia utiaji saini wa mkataba mkubwa na wa kati baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni tatu za uchimbaji madini kutoka nchini Australia.
Rais Dk. Samia alisema kuwa mikoa ya Lindi na Morogoro ipo katika ukanda wa madini kinywe na Mkoa wa Songwe uko katika ukanda wenye madini adimu ndio maana miradi iliyowekwa saini iko katika Wilaya za Lindi, Ulanga na Songwe.
“Utafiti wa madini ya kinywe na madini adimu ulianza tangu mwaka 2000 kupitia kampuni mbalimbali ambapo hadi sasa kuna kiasi cha tani milioni 67 zenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya kinywe yaliyogundulika katika kijiji cha Chilalo ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18, tani milioni 63 zenye wastani wa asilimia 7.6 yaliyogundulika katika kijiji cha Epanko nayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 18, tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.8 zenye madini adimu yamegundulika katika kijiji cha Ngwala ambayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 20 madini hayo ya kinywe na adimu yapo katika orodha ambayo kwa sasa yanajulikana kama madini muhimu duniani kwa kuwa yanahitajika sana katika teknolojia mpya ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo hutumika kutengenezea betri za magari, vifaa vya kieletriniki na mitambo mbalimbali,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa kufuatia uwepo wa madini hayo nchini, wawekezaji wakubwa duniani wameonesha kuvutiwa na Tanzania na kuwa hivi karibuni wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Marekani nchini, Kamala Harris walizungumzia umuhimu wa madini hayo pamoja na mradi wa Nikeli wa Kabanga na kiwanda cha usafishaji madini kitakachojengwa Kahama.
Rais Samia alisisitiza: “Katika siku zijazo nchi yetu itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini haya na hivyo kuvutia uwekezaji mahiri, vilevile kwa kutumia nafasi yetu kijiografia ambayo tumezungukwa na nchi nane ambazo baadhi zina madini kama haya fursa hiyo itatufanya Tanzania kuzidi kutunufaisha hasa kwa kuwa tutakuwa na viwanda vya kuchakata madini hayo hapa lakini pia tuna njia za kuaminika za kusafirisha madini hayo,” amesema.
Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema kuwa miradi hiyo ya madini ni kielelezo tosha kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameamua kwa dhati kuisimamia sekta ya madini na hivyo ukuaji wa sekta ya madini katika mchango wa Pato la Taifa umeongezeka zaidi katika kipindi kifupi ambapo Julai hadi Septemba 2022 sekta ya madini imeshachangia asilimia 9.7 ikiwa ni asilimia 0.3 kufikia lengo lililowekwa katika malengo ya Taifa.
“Sekta hii, Mhe. Rais umeilea na imendelea kuwa tegemeo kubwa katika mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kutuletea fedha za kigeni hapa nchini. Miradi hii yote ambayo leo imesainiwa italeta mtaji kutoka nje ya nchi jumla ya dola za Kimarekani milioni 667 hii ni miradi mikubwa na jambo la maana sana Mhe. Rais wakati dunia inahangaika kutafuta madini ya mkakati, miradi yote tuliyosaini leo hapa ni madini ya mradi wa kimkakati ambayo dunia inayahitaji,” alisema Waziri Biteko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Serikali ya Majadiliano, Prof. Palamagamba Kabudi alisema Tanzania imejaliwa kuwa na madini mbalimbali na hivyo kampuni ambazo Serikali inaingia nayo mkataba wa uchimbaji wa madini ni Picklayer Earth Ltd kutoka Australia na kupitia kampuni mbili zilizoundwa kwa ubia za Mamba Minerals Corporations itakayojihusisha na uchimbaji wa madini na Mamba Refinery Corporations itakayojihusisha na uchenjuaji wa madini na kuwa kampuni hizo mbili Serikali ya Tanzania ina hisa ya asilimia 16 isiyofifishwa.
Prof. Palamagamba alisema: “Gharama za uwekezaji za awali katika mradi huu ni dola za Marekani milioni 439 na katika maoteo ya mwanzo tuliyofanya mradi huu utakuwa Ruangwa mkoani Lindi kwa miaka 18, tunatarajia thamani ya mauzo ghafi ya madini haya ya Kinywe yatakuwa dola za kimarekani bilioni 1 na milioni 860.
“Kwa mgawanyo tuliouweka katika mizania mgawanyo mwekezaji na mbia wetu yeye atapata dola milioni 389 ambayo ni sawa sawa na asilimia 47 na Serikali itapata dola milioni 437 ambayo ni sawasawa na asilimia 53,” amesema..
Prof. Kabudi alitaja kampuni ya pili ambayo Serikali inaingia nayo mkataba ni Evolution Energy Minerals Ltd kutoka nchini Australia kuhusu mradi wa uchimbaji wa madini ya Kinywe wilayani Ruangwa mkoani Lindi kupitia Kampuni ya ubia ya Kudu Graphite ambapo Serikali itakuwa na umiliki wa asilimia 16 ya hisa huku mwekezaji wa asilimia 84, na gharama za uwekezaji za awali katika kampuni hiyo ni dola za Marekani milioni 100 na taarifa za awali za maoteo ni kuwa Serikali itapata asilimia 51 na wawekezaji asilimia 41.
Aidha, Kampuni ya tatu ni EcoGraf kuhusu uendelezaji wa mradi wa uchimbaji wa madini ya Kinywe uliopo wilayani Ulanga mkoani Morogoro kupitia Kampuni ya ubia ambayo imeshaundwa ya Cheater Tansgraphite Ltd ambayo Serikali itakuwa na asilimia 16 ya hisa isiyofifishwa na kampuni itakuwa na uwezo wa kumiliki hisa 84, ambapo gharama ya uwekezaji katika ni dola za Marekani 121, 700,000 na kampuni itapata asilimia 49 ya magawanyo huku Serikali ikipata asilimia 51.
Aidha, mikataba iliyosainiwa ni ya aina tatu ambayo ni mikataba wa makubaliano ya msingi kuhusiana na umiliki wa magawanyo wa faida za kiuchumi, mkataba wa wana hisa na mkataba wa t ambao ulishasainiwa wa katiba za kampuni.
Mkurugenzi wa Evolution Energy Limited, Phil Hoskins ambao wanahusika na mradi wa Chilalo, Ruangwa, Lindi alisema kuwa anaikaribisha Serikali ya Tanzania kuwa mmiliki mwenza na kuwa katika ushirikiano mpya wenye ushiriki wa moja kwa moja wa mradi wa uchimbai wa madini ya kinywe.
“Huu ni mwanzo mpya wa uwazi na kufanyakazi kwa manufaa yetu wote ikiwa ni pamoja na watu wa Wilaya ya Ruangwa na Watanzania wote kwa ujumla hivyo tunajipanga kufanya kazi vizuri zaidi ili kila mmoja ashiriki na aweze kufanikiwa,” alisema Hoskins.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa EcoGraf Limited, Andrew Spinks alisema kuwa anamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa madini utakaotekelezwa katika Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na pia wanatarajia kufanyakazi na Serikali katika ushirikiano huo mpya wa utekelezaji wa mradi huo wa madini. Aidha, kampuni yake imekuwa ikitekeleza miradi ya madini wilayani humo kwa miaka 10 sasa.