*Ni katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024
Na Denis Sinkonde, Songwe
Ikiwa imebakia miezi kadhaa Tanzania kuingia katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua Wenyeviti wa Vitongoji, Mitaa na vijiji, vijana wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) wilayani Ileje mkoani Songe nwametakiwa kujiandaa kugombea nafasi hizo ili kusimamia miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.
Wito huo umetolewa Aprili 17,2023 na Katibu wa Chama hicho wilayani humo, Hassan Lyamba wakati akizungumza na vijana wa chama hicho katika ukumbi wa CCM uliopo Itumba.
Lyamba amesema vijana ndio nguzo kuu ya chama hivyo ni wajibu wao kujiandaa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 kugombea nafasi za uenyekiti wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ili kukimbiza shughuli mbalimbali za maendeleo yaliyokusudiwa.
“Lengo la chama ni kushika dora, vivyo hivyo vyama pinzani vinahitaji kushika dora, ili kuendelea kuaminika na wananchi vijana mnatakiwa kuyasema yote yanayofanywa na serikali kupitia chama CCM,” amesema Lyamba.
Lyamba ameongeza kuwa vijana wa CCM wanatakiwa kuendana na mabadiliko ya siasa ikiwa ni pamoja na kujenga hoja pindi wanapokuwa majukwaani kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kwa nini waichague serikali inayoongozwa na chama hicho.
Hata hivyo, katibu huyo amesema vijana wanapaswa kupeana fursa za kiuchumi ili kujiongezea kipato kwa lengo la kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana CCM wilayani humo, Diana Ngabo amesema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 vijana watakuwa mbele kugombea nafasi hizo kwa kuangalia wenye sifa na watakaosimamia Ilani ya CCM.