Na Clara Matimo, Mwanza
Katika kukabiliana na mlipuko wa homa inayosababishwa na Virus vya Marburg mkoani Mwanza, mkoa huo umejiandaa kwa tiba na kinga ikiwemo kutoa elimu kwa wanachi kupitia vyombo vya habari na matangazo ya mtaani ili kuhakikisha wanaelewa jinsi ya kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Pia mkoa huo umeandaa mazingira ya kuwatibu watakaobainika wana maambukizi kwa kutenga maeneo maalum yatakayotumika kuhudumia wagonjwa wa ugonjwa wa Virus vya Marburg na kuwapa mafunzo wataalamu katika nyanja mbalimbali za afya ili kutoa huduma kwa wagonjwa endapo ugonjwa huo utaingia ndani ya mkoa huo.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Mwanza, Renard Mlyakado leo Machi 24, 2023 wakati akizungumza kwenye kikao kilichokutanisha wadau mbalimbali kutoka makundi tofauti tofauti wakiwemo viongozi wa dini na wavuvi kilicholenga kuwaelimisha kuhusu ugonjwa huo, athari zake, dalili, jinsi ya kujikinga na unavyoambukizwa.
Mlyakado amesema hadi sasa jumla ya watumishi 94 kutoka halmashauri nne kati ya nane zilizopo mkoani humo wamekwishapewa mafunzo mahususi jinsi ya kuhudumia wagonjwa wa ugonjwa huo huku akibainisha kwamba mafunzo hayo yanaendelea kutolewa katika halmashauri zote na mahala pa kazi.
Amesema ugonjwa huo unaambukizwa kwa haraka kutoka mtu mmoja aliye na Virus vya Marburg hadi mwingine kwa kugusa majimaji ya mwili mfano damu, matapishi, mkojo, jasho, machozi na kamasi,kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kwa ugonjwa huo, kugusa godoro au nguo zilizotumiwa na mgonjwa mwenye ugonjwa huo, kuchomwa sindano au vifaa visivyosafi na salama vilivyotumiwa na mgonjwa wa Marburg, kugusa mizoga au kula wanyama pori kama vile nyani na sokwe ama matunda yaliyoliwa nusu na wanyama.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Mwanza dalili huanza kujitokeza kati ya siku mbili hadi 21 baada ya mtu kupata maambukizi ikiwemo homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, mwili, misuli na viungo vya mwili, kuharisha na kutapika kunakoweza kuambatana na damu, vipele mwilini, kuvia damu chini ya ngozi au kutokwa na damu puani, mdomoni,machoni na masikioni.
Mlyakado amewataka wananchi kuwa makini katika kujikinga na ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa afya kwani hauna tiba maalum wala chanjo bali mgonjwa hupatiwa matibabu kulingana na dalili alizonazo.
“Halmashauri zote zilizopo mkoani humu zimekwishatenga maeneo maalum ya kuhudumia wagonjwa wa ugonjwa wa Virus vya Marburg Wilaya ya Nyamagana ni hospitali ya wilaya na SRRH, Ilemela hospitali ya Wilaya Kabusungu, Kwimba zahanati ya Mwamajila, Misungwi Zahanati ya Igokello, Buchosa ni hospitali ya Wilaya, Ukerewe hospitali ya Nansio na Bwisya, Sengerema ni zahanati ya Mwabaluhi na Magu ni zahanati ya John Mongela,” amesema Mlyakado.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Mbunifu wa Majengo Chagu Ng’homa amesema “Tunatakiwa tupambane na hili janga bila kuleta taharuki kwa jamii natambua kwamba Ugonjwa wa Virus vya Marburg husababisha unyanyapaa na athari za kisaikolojia kwa waathirika na familia zao.
“Pia ni gharama kubwa kuhudumia wagonjwa wa ugonjwa huo lakini ni lazima tushirikiane tusiwe na hofu Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali hasa kule Mkoani Kagera ulikoanzia hii inatupa matumaini na hatujatangaziwa ongezeko la wagonjwa,” amesema Ng’homa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk.Thomas Rutachunzibwa amesema endapo mtu atakuwa na dalili moja wapo kati ya zilizotajwa au akiona mtu kwenye dalili hizo asimnyanyapae bali waende au wawashauri kwenda haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, watoe taarifa mapema kwenye vituo vya huduma za afya, ofisi ya serikali ya mtaa au kijiji.
“Tangu ugonjwa wa Marburg ulipoingia nchini Machi mwaka huu katika mkoa jirani wa Kagera na kutangazwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Machi 21, 2023 tulianza kujipanga kwa kuweka mikakati ya kuzuia usiingie ndani ya mkoa wetu pamoja na kuandaa mazingira ya kuwatibu watakaobainika wana maambukizi endapo utaingia mkoani kwetu maana mkoa wa Mwanza unapokea wageni wengi pia tuko jirani na Mkoa wa Kagera,”amesema Dk. Rutachunzibwa na kuongeza
“Tunawategemea sana viongozi wa dini kuwaelimisha wananchi kuhusu janga la ugonjwa huu mkiwa kwenye nyumba zenu za ibada waambieni waumini wenu wajue kwamba ugonjwa huu upo mkoa jirani wa Kagera, dalili zake na jinsi ya kujikinga ili wote kwa pamoja tushiriki katika kujikinga na kuudhibiti usiingie mkoani kwetu, matarajio yangu elimu mliyoipata hapa leo mtaanza kuitoa leo misikitini, kesho na kesho kutwa wenzetu wakristo nao wataendelea kuitoa kwenye makanisa yao,”amesema Dk. Rutachunzibwa.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alitoa taarifa kwa umma Machi 21, 2023 kwamba uchunguzi wa kimaabara uliofanyika katika Maabara ya Taifa ya Jamii umethibitisha uwepo wa ugonjwa wa Homa inayosababishwa na Virus vya Marburg mkoani Kagera ambapo kulikuwa na jumla ya wagonjwa nane kati yao watano walifariki na watatu wanaendelea na matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoandaliwa mkoani humo.