Na Gustafu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amewaapisha Wakuu wa Wilaya wapya walioteuliwa hivi karibuni na kuwataka waende kutatua kero za wananchi pamoja na kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo.
Hafla hiyo imefanyika Januari 30, 2023 Mjini Kibaha ambapo miongoni mwa wakuu wa Wilaya walioapishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Josephu Kolombo na Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye.
Katika hafla hiyo, Kunenge ametoa maagizo mbalimbali ambapo moja ya maagizo hayo ni kuhakikisha wanakwenda kuwatumikia wananchi kwa kutatua kero zao na hata kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Kunenge amesema kuwa viongozi walioteuliwa na Rais Dk. Samia Suluhu ni watumishi wa wananchi ambao wameridhia CCM kushika dola kwakuwa wanaimani ndio chama kinacholeta maendeleo.
Amesema wananchi na CCM wameingia mkataba maalum ambao ni ilani na kwamba kazi ya viongozi ni kutekeleza yale yote yaliyomo kwenye ilani ili kusudi wananchi waendelee kuwa na imani na chama chao.
Mbali na hilo lakini pia Kunenge amewataka wakuu hao wa wilaya kuangalia vipaumbele vya Rais Dk.Samia ambavyo ni kutangaza Demokrasia, Utawala wa Kisheria na Utawala bora.
Aidha, Kunenge aliongeza kuwa Serikali kazi yake ni kutoa huduma za jamii ikiwemo Barabara, Umeme, Maji, Elimu na Afya na kwamba Wakuu wa Wilaya lazima wahakikishe huduma hizo zinapatikana katika maeneo yao.
Kunenge alisema wakuu wa Wilaya ili waweze kufanyakazi zao vizuri ni lazima washirikiane na taasisi zote za umma pamoja na Halmashauri husika ambapo kwa kufanya hivyo itasaidia kuleta ufanisi katika usimamizi wa mapato.
“Tujitahidi sana kuweka mazingira bora ya uwekezaji , kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ,matatizo ya uvamizi wa ardhi lakini msimuonee mtu wala msimpendelee mtu,”alisema Kunenge
Hatahivyo, pamoja na mambo mengine Kunenge ,aliwaagiza viongozi wote waliopo ndani ya Mkoa kwenda kukemea vikali masuala ya jinsia moja(Ushoga),Ubakaji,ukabaji,matumizi ya madawa ya kulevya na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia huku akiwaomba viongozi wa dini kusaidia katika kukemea vitendo hivyo katika nyumba zao za ibada.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Zuwena Omary,aliwapongeza wakuu wa Wilaya walioteuliwa na kusema kilichobaki ni kuendelea kuchapakazi ili waendelee kuaminiwa ambapo amewaomba kufanyakazi kwa ueledi .
Zuwena,alisema waende kuisimamia miradi ya maendeleo pamoja na kutangaza kazi nzuri zilizofanywa chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kusema ipo miradi mingi imefanyika lakini haijatangazwa.
“Nendeni mkadhibiti mapato na hasa kuwabana wale wote wanaofanya makusudi ya kutorosha mapato na katika makusanyo zingatieni kutumia Posi lakini hakikishe mnatumia vyombo vya habari kutangaza miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali,” alisema Zuwena
Hatahivyo, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwishehe Mlao ,amewataka waende kujifunza kwa haraka na kujua hali ya kisiasa zilivyo katika maeneo yao na sio kwenda kubeba wagombea .