Na Hadia Khamis, Mtanzania Digital
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ameiagiza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kujielekeza katika kubuni teknolojia nyepesi zinazowagusa Watanzania wengi ikiwemo za kutengeneza vyakula vya mifugo kama kuku na samaki kwa bei nafuu Ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa vyakula hivyo ambavyo vimekuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi.
Ulega ametoa wito huo Julai 5, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alipotembelea maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba ambapo amesema zipo sababu kadhaa zinazopeleka changamoto hiyo ikiwemo matatizo yanayoendelea ulimwenguni lakini pia kuongezeka kwa mahitaji ya binadamu hivyo kusababisha vyakula hivyo kupanda bei.
“Watanzania wafike Katika Banda letu ili waweze kujifunza zaidi katika suala zima la uwekezaji,”amesema Ulega .
Alisema kama wizara wanamuunga mkono Rais Samia Suluuhu Hassan kwa kufungua milango ya Uwekezaji nchini na kwamba hiyo iende sambamba na Watanzania kujipanga kupokea uwekezaji huo Ili na wao wanufaike na wawekezaji wanufaike.
Alisema tumetengeza vizimba Kwa ajili ya vijana zaidi ya vijana 1500 kutoka Ziwa Viktoria watapatiwa mafunzo ya kutengeneza samaki aina ya sato, tani laki nane ambavyo vitazalisha zaidi ya shilingi Bilioni nane ikiwa ni sehemu ya kutoa ajira na wao kujiongezea vipato.