26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tunatambua mchango wa Waganga wa tiba asili katika elimu- Kafulila

Na Samwel Mwanga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amesema Serikali inatambua mchango wa Waganga wa Tiba Asilia na Tiba Mbadala katika sekta ya elimu mkoani humo.

Kafulila amebainisha hayo Aprili 7, 2022 wakati akizungumza katika kongamano la Waganga wa tiba asili lililofanyika kwenye Uwanja wa michezo wa CCM mjini Bariadi na kuhudhuriwa na waganga kutoka wilaya zote za mkoa huo.

Mifugo iliyotolewa na Waganga wa tiba asilia na tiba mbadala kuchangia sekta ya elimu katika mkoa wa Simiyu na kukabidhiwa kwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu, David Kafulila.

Amesema kuwa mafanikio ya mkoa huo katika sekta ya elimu yamechangiwa na wadau mbalimbali na waganga hao ni sehemu hiyo kwani wamefanya kazi kubwa ya kutoa michango mbalimbali .

Amesema waganga hao wamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha kuwepo kwa makambi ya kitaaluma kwa wanafunzi walioko kwenye madarasa ya mitihani yakiwemo darasa la nne,darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita.

Amesema mbali na hilo pia wamekuwa wakitoa michango kwa ajili ya kuwapatia motisha  chanya walimu wa shule za msingi na sekondari waliofanya vizuri katika kufundisha masomo yao katika mitihani ya kitaifa sambamba na kuwapa motisha wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani yao ya kitaifa.

Kafulila amesema kuwa mara baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa huo mwaka 2020 alikuta mkoa huo ukiwa na nafasi ya tano kwa matokeo ya kidato cha nne lakini kwa matokeo ya mwaka 2021 yaliyotangazwa mwaka huu kwa kidato hicho umeshika nafasi ya tatu hivyo wanajipanga kushika nafasi ya juu yaani namba moja mwaka huu.

“Michango hii mnayoitoa katika sekta ya elimu hizi salamu zenu zinafika kwa viongozi wa ngazi za juu wa serikali ambao ni Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na wakuzipeleka ni mimi mkuu wenu wa mkoa,” amesema Kafulila.

Amefafanua zaidi kuwa kutokana na matokeo hayo mazuri ya mwaka jana katika kuwapatia motisha walimu na wanafunzi waliofanya vizuri watatoa zawadi zenye thamani ya Sh milioni 81.

Aidha, katika kutambua mchango wa waganga hao katika sekta hiyo, Kafulila amekabidhi vyeti vya kutambua mchango huo kwa waganga hao katika wilaya za mkoa huo ambazo ni Maswa, Bariadi, Itilima, Busega na Meatu.

Awali, Mlezi wa Waganga hao mkoa wa Simiyu, Shemsha Mohamed ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Simiyu alimkabidhi Mkuu wa mkoa huo, mchango wa ng’ombe 13 na mbuzi 53 zilizotolewa na waganga hao kwa hiari yao kuunga mkono jitihada za mkoa huo katika sekta ya elimu ikiwa ni sehemu ya kuchangia motisha kwa walimu na wanafunzi.

Naye Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asilia na tiba mbadala mkoa huo, Dk. Shija Limbe amesema kuwa michango yote wanayoitoa katika shughuli za maendeleo ikiwemo hiyo ya elimu inatolewa kwa hiari yao bila kulazimishwa na mtu yeyote.

Pia amekabidhi kiasi cha fedha taslimu Sh 1,420,000 zilizochangwa na waganga hao katika kongamano hilo huku ahadi zikiwa Sh 300,000 ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za uongozi wa mkoa huo katika sekta ya elimu.

“Hii michango tunayochangia katika shughuli za maendeleo katika mkoa wetu hususan sekta ya elimu tunaitoa kwa hiari yetu na hii mifugo na fedha hatujalazimishwa na mtu maana kuna maneno maneno uanasemwa tumelazimishwa ni uongo na hatuwezi kukatishwa tamaa sisi tunajitambua maana elimu inawagusa watoto wetu,”amesema Dk. Limbe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles