25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Makala awaonya wanaofanya biashara maeneo yaliyokatazwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, ameagiza kuondolewa kwa wafanyabiashara katika barabara zote zinazoingia na kutoka linapojengwa soko la kisasa la Kariakoo ili zibaki wazi kumwezesha mkandarasi kufanya kazi kwa ufanisi.

Ametoa agizo hilo wakati wa usafi wa pamoja unaofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambao ulifanyika katika barabara zinazoingia Soko la Kariakoo na kuitaka halmashauri ya jiji kuimarisha ulinzi katika barabara hizo.

“Nafasi kwenye masoko bado zipo wafanyabiashara wasilianeni na mamlaka husika ili mpatiwe maeneo mtakayofanya biashara bila usumbufu,” amesema Makala.

Zoezi hilo pia lilihusisha wafanyakazi wa Benki ya NMB ambapo Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, amesema wanaunga mkono kampeni ya mkuu wa mkoa ya kusafisha na kupendezesha Jiji la Dar es Salaam.

“Tunamuunga mkono mkuu wa mkoa kwenye kampeni yake kwa sababu wateja wetu ni sehemu ya jamii inayotuzunguka hivyo tunawahamasisha na wananchi wote ili tuliweke jiji letu liwe safi, tunataka Jiji la Dar es Salaam litoke kwenye namba sita liwe namba moja katika usafi,” amesema Richard.

Meneja huyo ametoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kujitoa kufanya usafi badala ya kusubiri kushinikizwa na viongozi kwani kwa kufanya hivyo wataepuka magonjwa na kulifanya jiji hilo lizidi kuwa kivutio cha biashara na utalii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya kuzoa taka ya Kajenjere, Mathew Andrew, amesema wataweka mapipa ya kuhifadhi taka kuhakikisha jiji linakuwa safi.

“Jambo la usafi linaanza na mtu mwenyewe sisi kama wakandarasi tutahakikisha taka zote zinazozalishwa zinazolewa na kupelekwa dampo, wananchi waelewe pia taka nyingine ni fursa hivyo elimu iendelee kutolewa,” amesema Andrew.

Katika zoezi hilo pia meza zilizokuwa zimepangwa na wafanyabiashara katika barabara zinazoingia na kutoka linapojengwa soko la kisasa la Kariakoo ziliondolewa huku mkuu wa mkoa akiwaonya watendaji wasio waaminifu wanaopokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara ili kuwaruhusu kufanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles