Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa siku 60 kwa wale ambao hawajalipa kodi ya pango la ardhi na waliopimiwa viwanja na hawajamilikishwa kuwasilisha maombi ya kumilikishwa viwanja hivyo.
Imesema wasipofanya hivyo Serikali itachukua hatua za kisheria ikiwemo kufuta umiliki, kupiga mnada na kumilikisha viwanja vilivyopimwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji.
Hayo yameelezwa leo Februari 24, mwaka huu na Afisa Ardhi Mkuu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Biswalo Makwasa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu umiliki ardhi kwa viwanja vilivyopimwa pamoja na ulipaji wa kodi ya pango la ardhi.
Amesema wamiliki wa ardhi wanakumbushwa wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi ya pango la ardhi.
Afisa Ardhi huyo amesema wizara imetoa muda wa siku 60 kuanzia Februari 5, mwaka huu kuhakikisha wale waliopimiwa viwanja wanawasilisha maombi ya kumilikishwa na wale wenye milki za ardhi wawe wamelipa kodi ya pango la ardhi.
Amesema mmiliki ambaye hatalipa kodi serikali itachukua hatua za kisheria ikiwemo kufuta umiliki, kupiga mnada na kumilikisha viwanja vilivyopimwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami ametoa rai kwa Watanzania kulipa kodi ya pango la ardhi kwa njia ya kieletroniki kwa kutumia simu kwani ni rahisi na ni rafiki.
Amesema bado kumekuwa na changamoto kwa Watanzania kushindwa kutofautisha kati ya kodi ya pango la ardhi na kodi ya majengo ambapo amesema kodi ya majengo inakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwa sasa inakusanywa kupitia luku kwenye umeme.
Amesema kodi ya pango la ardhi inakusanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia mifumo ya Kieletroniki hivyo amewaomba wananchi anaedaiwa kodi hiyo kulipe.
Pia amesema wizara ina mkakati wa kwenda nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinachodaiwa wanapeleka hati ya madai ambapo amedai hali hiyo inaleta tija.
Amesema kwa Mkoa wa Dodoma ulipaji wa kodi ya ardhi umeongezeka ambapo katika kipindi cha Desemba mwaka jana wiki mbili za kwanza ulipaji wa kodi ulikuwa wamiliki 200 lakini baada ya kuanza zoezi la kupeleka hati za madai walifika mpaka 200 kwa wiki na mapato yalitoka Sh milioni 40 kwa wiki mpaka milioni 102.
“Kingine ambacho tunachokifanya tunakituo cha Mawasiliano kwa wananchi kinatoa huduma watumishi wanawasaidia wananchi namna ya kulipia lakini kinasaidia pia kutunza taarifa, lakini pia mfumo unarekodi ukifika taarifa wahusika wanakumbushwa,”amesema.