*Atoa witoa kwa Wanaume kujitokeza kupima
*Ahimiza Tanzania kujitegemea kwa kutunisha mfuko wa ATF
*Ataka UKIMWI kutokomezwa kabla ya 2030
Na Faraja Masinde, Mbeya
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amehimiza kuendelea kwa mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI ili kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Ijumaa Novemba 26, wakati akifungua Kongamano la siku mbili la Kisayansi mkoani Mbeya ikiwa ni katika kueleka Wiki ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Desemba Mosi, ambapo kitaifa inafanyika mkoani humo.
Waziri Mkuu amesema kuwa Tanzania inaweza kufikia ndoto hiyo ya kutokomeza UKIMWI hata kabla ya muda iliyojiwekea iwapo kila mmoja atashiriki kikamilifu kwenye nafasi yake.
“Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imekuwa ikifanya kazi nzuri sana sana na nimpongeze Mkurugenzi Mtendaji, Dk. Leonard Maboko, lakini lazima tutambue kuwa malengo ya kutokomeza ugonjwa huu ifikapoa mwaka 2030 au kabla inawezekana tu iwapo kila mtu atawajibika katika nafasi yake kikamilifu, uwe ni mkuu wa Wilaya, kijiji kila eneo ambalo mtu ni kuongozi awe mstari wa mbele.
“Mfano, ukiangalia takwimu zinaonyesha kwamba wanaume wako nyuma sana kwenye kujitokeza kupima, badala yake wamekuwa wakisubiri majibu ya wenzi wao tu ndio wayatumie hayo kama kielelezo jambo ambalo linadhorotesha jitihada za kutokomeza ugonjwa huu.
“Hivyo, niwahimize wanaume wenzangu tujitokeze kwa wangi kwenye vituo mbalimbali vya afya kwa ajili ya kujua hali zetu kwani kuna faida sababu hata kama utakubwa umeambukizwa basi utaweza kuanza matumiza ya dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huu mapema na utapata ushauri ule nini kwa ajili ya kuimarisha afya yako, hivyo wanaume wenzangu tujitokeze kupima ili kufikia malengo tuliyojiwekea kama taifa,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI lakini ni muhimu zaidi juhudi hizo zikiambatana na kujitegemea kwa Serikali.
“Kama tunavyofahamu kwamba Tanzania tumeanzisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI (ATF) ambao utatusaidia katika mapambano haya, hivyo serikali itaendelea kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali ikiwamo sekta binafsi kuchangia mfuko hu muhimu.
“Itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI pamoja na kutafuta vyanzo vya uhakika zaidi vya kutunisha mfuko huo, ninawahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika kupambana na tatizo hili la UKIMWI,” amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kwa niaba ya Serikali kuwashukuru wadau wote wa maendeleo kwa kuendelea kufanya kazi na serikali katika utekelezaji wa miradi ya kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI nchini.
“Nawapongeza wadau mbalimbali wakiwamo Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake(UN WOMEN) ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa adhma ya serikali inafanikiwa, na ndiyo maana mwamko wa wanawake kwenda kupima na kutambua hali zao umekuwa mkubwa ikilinganishwa na wanaume,” amesema Majaliwa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko, amesema kongamano hilo la siku mbili ni fursa ya kuweza kutafakari walikotoka ili waweze kuendelea kutekeleza afua za VVU na UKIMWI.
Amesema kongamano hilo linawapa fursa nzuri ya kupata takwimu zinazowasaidia kuboresha utendaji kazi ambapo ametoa mfano mwaka 2016/17 walifanya tafiti na kubaini wanaume wako nyuma katika suala zima la upimaji hivyo wanatakiwa wahamasishwe ili nao wajitokeze kwa wingi kupima.
“Makongamano kama haya ndiyo yamekuwa msaada kwa TACAIDS kupiga hatua ikiwamo kuandaa tafiti mbalimbali, hivyo tayari maandalizi yamekamilika kwa ajili ya utafiti wa mwakani,” amesema Dk. Maboko.
Naye, Mwakilishi wa Mratibu Mkazi wa PEPFAR Tanzania, Dk. Hiltruda Temba ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira ya dhati ya kutokomeza VVU na UKIMWI nchini pamoja na kuendelea kutoa kipaumbele katika huduma muhimu za kinga pamoja na utekelezaji mzuri wa afua za UKIMWI.
Aidha, Dk. Hiltruda amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira yake ya dhati ya kufikia malengo ya kuwa na asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao za maambukizi, asilimia 95 ya watu wanaofahamu hali zao za maambukizi ya VVU wanapata tiba na asilimia 95 ya waliotumia dawa za ARV wamefanikiwa kupunguza kiasi cha maambukizi.
Dk. Hiltruda amesema PEPFAR na wadau wengine wa maendeleo wanaahidi kuendelea kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kufikia malengo yake ya kimkakati kama yalivyoainishwa kwenye mkakati wa nne wa Taifa wa VVU na UKIMWI.
Kilele cha maadhimiho ya Wiki ya UKIMWI kitaifa kinatarajiwa kufanyika Desemab Mosi katika Uwanja wa Ruandanzovwe jijini Mbeya ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katika Maadhimisho hayo, Kauli mbiu ya Mwaka huu inasema “Zingatia usawa. Tokomeza UKIMWI. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”