28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Muleba wapongezwa kwa kushiriki maendeleo

Renatha Kipaka, Muleba.

Wananchi wa Kijiji cha Kyota kata ya Kimwani wilayani Muleba mkoani Kagera wamepongezwa kwa jitihada wanazochukua katika kuhakikisha kuwa wanachangia maendeleo yao hususan kwenye nyanja ya miundombinu ya elimu na barabara.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Kyota, wananchi wamehimizwa kuchangia michango ya chakula ili kuwawezesha wanafunzi kupata huduma ya hiyo shuleni ikiwa ni sehemu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila ametoa pongezi kwa viongozi wa kijiji hicho kwa kuweka jitihada zao katika ujenzi wa shule mpya ya sekondari inayojengwa iliyofikia hatua ya linta huku akiwasihi kuwa ipo haja ya kuanza kuchangia chakula ili watoto waweze kupata chakula shuleni.

“Nitumie nafasi hii kuwaeleza kwamba Serikali imetoa Sh milioni 60 ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na fedha tayari imeshawekwa kwenye akaunti pia mmewekewa fedha ya kumalizia maboma mliyoyainua kwa nguvu zenu na mpaka sasa mabati yamenunuliwa. Kwa hiyo ongezeni nguvu kazi ili fedha mliyopewa iweze kubaki na kuwasaidia kujenga vyoo,” amesema Nguvila.

Hata hivyo, ameendelea kusema kuwa wananchi wa kijiji cha Kyota na wilaya ya Muleba kwa ujumla wanatakiwa kuwekeza katika kilimo ili kuweza kusaidia kuepuka na janga la njaa.

“Ukanda wa Kimwani ni moja ya maeneo yanayotegemewa kwa chakula wilayani Muleba, hasa kilimo cha mpunga. Kwa sehemu kubwa mchele unatoka Kimwani na ndio unalisha wilaya ya Muleba niwaombe wananchi limeni sana tupate hazina ya chakula cha kutosha kwa ajili ya faida yenu na faida ya wilaya kwa ujumla,” amesema Nguvila.

Wakitoa kero mbalimbali wananchi hao wamelalamika juu ya ukosefu wa elimu sahihi juu ya mikopo inayotolewa na Halmashauri.

Ukosefu wa umeme wa uhakika kwani umekuwa ukikatika mara kwa mara, ubovu wa barabara kuanzia Kyota hadi Kagulamo na kero juu ya bei za huduma za maji.

Aidha kwa upande wa kero za barabara Kaimu Meneja wa TARURA, Potency Deogratias amewaeleza wananchi kuwa kuhusiana na changamoto hiyo ya Kyota mpaka Kagulamo yenye urefu wa kilomita 6, zabuni imeshatangazwa na tayari amepatikana Mkandarasi ambaye atakwenda kuanza kazi ya ukarabati wa barabara hiyo ili kuweza kutatua kero katika eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles