Na Ramadhan Hassan, Dodoma
KATIKA kipindi cha robo ya pili ya mwaka (Aprili- Juni) 2021 uchumi wa Tanzania umeongezeka kwa asilimia 4.3 ikiwa ni pointi za asilimia 0.3 zaidi ya ilivyokuwa katika robo ya pili ya mwaka 2020.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 12,2021 na Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Daniel Masolwa wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma.
Masolwa amesema pato la taifa kwa bei ya miaka husika liliongezeka hadi shilingi trilioni 39.2 kutoka Sh 37.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Amesema pato halisi la taifa liliongezeka hadi Sh trilioni 33.4 mwaka 2021 kutoka Sh trilioni 32.0 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2021 shughuli za Habari na Mawasiliano iliongoza kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa asilimia 12.3 ikifuatiwa na uzalishaji wa umeme asilimia 12.1.
“Huduma nyingine za jamii zikijumuisha Sanaa na Burudani na shughuli za Kaya katika kuajiri (asilimia 10.8 malazi na huduma za chakula asilimia 10.1,usambazaji maji asilimia 8.4, uchimbaji wa madini na mawe asilimia 7.3,”amesema Masolwa.
Katika hatua nyingine, Masolwa ambaye ni Mkurugenzi wa takwimu za uchumi amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndio yenye jukumu la dhamana hapa nchini na ina wajibu wa kutoa tafsiri sahihi ya takwimu mbalimbali.
Hatua hiyo imekuja kufuatia hivi karibuni kuwa na taarifa zinazoainisha Mikoa tajiri na maskini hapa nchini ingawa takwimu hizo zimetokana na chanzo sahihi lakini tafsiri yake inapotosha kwa kiasi kikubwa.
Amesema uchambuzi wa kubaini Mikoa maskini na tajiri unatakiwa utumie viashiria zaidi ya pato la Taifa ambapo viashiria vingine vinaweza kuzingatiwa ni pamoja na mfumuko wa bei, kiwango cha umaskini, elimu, afya, maji, miundombinu ya usafiri na masoko.