STOCKHOLM, SWEDEN
MCHEZAJI wa timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars), Michael Olunga, amefanikiwa kujiunga na klabu ya Djurgardens ya nchini Sweden.
Nyota huyo ambaye alikuwa anakipiga katika klabu ya Gor Mahia, mwaka jana alijirekodi video ambayo ilionesha kwamba anamtaka Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, amsajili katika klabu yake.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, amemalizana na klabu hiyo ya Sweden kwa mkataba wa miaka minne, huku uongozi wa klabu hiyo ukidai kwamba umeridhika na uwezo wa mchezaji huyo.
Mkurugenzi wa klabu hiyo, Bosse Andersson, amedai kwamba Olunga ameonekana kuwa mchezaji ambaye anapenda kujifunza na wanaamini atatoa mchango mkubwa kwao.
“Olunga ni mchezaji ambaye anajitoa kwa ajili ya timu, anajituma sana mazoezini na anapenda kujifunza kwa ajili ya baadaye.
“Kutokana na utaratibu wetu tunaamini tutampa nafasi kwa ajili ya kuonesha kile ambacho anacho ili aweze kujipatia nafasi ya kucheza soka katika klabu kubwa zaidi barani Ulaya na ndilo lengo lake,” alisema Anderson.
Olunga, ambaye anajulikana kwa jina la ‘Engineer’, jina ambalo alilipata wakati anasoma chuo pamoja na uwezo wake wa kucheza soka, amefurahi kujiunga na klabu hiyo, lakini amedai kwamba kasi yake itakuwa ndogo mwanzoni.
“Ninaamini nitaanza kwa kasi ndogo, lakini nikija kuzoea nitakuwa kwenye ubora wangu, tayari nimeanza kwa kucheza michezo ya kirafiki, lakini ninahisi kuwa nipo katika ubora sahihi kwa kuwa mambo ni mazuri hapa, kambi ipo vizuri,” alisema Olunga.