KAMPUNI ya utengenezaji vifaa vya michezo ya Nike imesitisha mkataba na uhusiano na bondia Manny Pacquiao, baada ya nyota huyo wa uzito wa juu duniani kuwashambulia wapenzi wa jinsia moja.
Bingwa huyo wa masumbwi ulimwenguni mwenye umri wa miaka 37, ambaye anagombea nafasi ya useneta katika bunge nchini Ufilipino, mwanzoni mwa wiki hii alisema kwamba ‘watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni wabaya kuliko wanyama’.
Kutokana na hali hiyo, kampuni ya NIKE imetoa tamko lake kwa kusema kuwa kauli ya bondia huyo ina ufinyu wa mawazo.
Katika tamko hilo, Nike inapinga ubaguzi wa aina yoyote ile na kwamba kampuni hiyo imejiwekea historia ya kuwaunga mkono na kutetea misimamo yake dhidi ya haki ya jamii ya wapenzi wa jinsia moja.
Kampuni hiyo inayojishughulisha na vifaa vya michezo imethibitisha kuvunja mkataba na uhusiano na bondia huyo.
Kauli hiyo ya Pacquiao aliitoa wakati alipokuwa akifanyiwa mahojiano kwenye runinga ambako awali alionekana kutojutia kauli yake hiyo, lakini baadaye katika akaunti yake ya Instagram akaitetea kauli hiyo kwa kusema kwamba alikuwa akisema ukweli kwa mujibu wa kilichoandikwa kwenye vitabu vya dini.
Hata hivyo, baadaye bondia huyo akaandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba alikuwa haishambulii jamii hiyo ya wapenzi wa jinsia moja.
Pacquiao anatarajiwa kuingia ulingoni kumkabili Mmarekani Timothy Bradley Jr mjini Las Vegas, Aprili mwaka huu.