BENDI ya YaMoto inatarajiwa kutumbuiza mashabiki na washiriki wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager, katika mashindano yatakayofanyika Februari 28, viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU).
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, ambao ndio wadhamini wakuu wa mbio hizo, Pamela Kikuli, alisema wamechagua bendi hiyo kwa kuwa wanaamini inaweza kuburudisha idadi kubwa ya watu wanaotarajiwa kuhudhuria mbio hizo.
Pia Kikuli alisema wasanii wanaochipukia kutoka Mkoa wa Kilimanjaro watapata fursa ya kutumbuiza katika jukwaa moja na bendi hiyo ili waonyeshe uwezo wao. Mbio hizo zinatarajiwa kuwa kivutio cha takribani washiriki zaidi ya 8,000 kutoka nchi zaidi ya 45.